Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
(1)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Imeundwa.
(2)Mtu hastahiki kuteuliwa kama mwanachama wa Tume ikiwa mtu huyo—
(a)ndani ya miaka mitano iliyopita, amehudumu au kugombea kiti kama—
(i)mbunge katika Bunge la Kitaifa au mwakilishi wadi katika bunge la kaunti; au
(ii)mwanachama katika idara ya uongozi wa chama cha kisiasa; au
(b)anahudumu katika ofisi yoyote ya Serikali.
(3)Mwanachama wa Tume hatahudumu katika ofisi nyingine ya umma.
(4)Tume ina wajibu wa kuendesha na kusimamia kura za maamuzi na uchaguzi katika shirika lolote ambalo wanachama wake wanachaguliwa au katika ofisi chini ya Katiba hii, na uchaguzi mwingine wowote kama ilivyoagizwa katika Sheria ya Bunge, na katika—
(a)usajili unaoendelea wa raia kama wapiga kura;
(b)ukaguzi wa mara kwa mara wa sajili ya wapiga kura;
(c)uwekaji mipaka katika maeneo bunge na wadi;
(d)kudhibiti mchakato ambao vyama hutumia katika kuteua wagombea wa uchaguzi;
(e)kusuluhisha mizozo ya uchaguzi, ikijumuisha mizozo inayohusiana au kutokana na uteuzi lakini isiyohusisha malalamishi kuhusu uchaguzi na mizozo inayotokana na kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi;
(f)usajili wa wagombea wa uchaguzi;
(g)elimu kwa wapiga kura;
(h)kuwezesha uchunguzi, usimamizi na tathmini ya uchaguzi;
(i)udhibiti wa kiwango cha fedha kinachoweza kutumiwa na mgombea au kwa niaba yake, au na chama katika uchaguzi wowote;
(j)uundaji wa kanuni za uchaguzi kwa wagombea na vyama vinavyogombea katika uchaguzi; na
(k)ufuatiliaji kuhusu ufuataji wa sheria inavyohitajika chini ya Kifungu cha 82 (1) (b) kuhusiana na uteuzi wa wagombea katika vyama.
(5)Tume itatumia mamlaka yake kutekeleza majukumu yake kulingana na Katiba hii na sheria ya kitaifa.