Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Saba · Uwakilishaji wa Watu

Kifungu cha 89

Kif.89

Uwekaji mipaka katika maeneo ya uchaguzi

(1)Kutakuwa na maeneo bunge mia mbili tisini kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge katika Bunge la Kitaifa kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 97 (1) (a).

(2)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itakagua majina na mipaka ya maeneo bunge kila baada ya muda usiopungua miaka nane na usiozidi miaka kumi na miwili, lakini ukaguzi wowote utakamilishwa angalau miezi kumi na miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa wabunge.

(3)Tume itakagua idadi, majina na mipaka ya wadi mara kwa mara.

(4)Ikiwa uchaguzi mkuu utafanyika ndani ya miezi kumi na miwili baada ya kukamilika kwa ukaguzi wa Tume, mipaka hiyo mipya haitazingatiwa kwa madhumuni ya uchaguzi huo.

(5)Mipaka ya kila eneobunge italinganishwa, kwa kiasi kiwezekanacho, na idadi ya wakazi katika eneo bunge hilo, lakini idadi ya wakazi katika eneobunge inaweza kuwa kubwa au ndogo kuliko idadi ya watu inayolingana na eneo hilo kwa namna ambayo imetajwa katika Ibara ya (6) ili kuzingatia—

(a)hali ya kijiografia na maeneo ya miji;

(b)jamii ya eneo lile, historia, uchumi na mahusiano ya kitamaduni; na

(c)mbinu za mawasiliano.

(6)Idadi ya wakazi katika eneobunge au wadi inaweza kuwa kubwa au ndogo zaidi ya idadi ya watu inayolingana na eneo hilo kwa kiwango kisichozidi —

(a)asilimia arobaini kwa majiji na maeneo yaliyo na idadi ya watu iliyotawanyika; na

(b)asilimia thelathini kwa sehemu nyingine.

(7)Katika kukagua mipaka ya maeneobunge na wadi, Tume-––

(a)itashauriana na wote wanaohusika; na

(b)itandelea kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba idadi ya watu katika kila eneobunge na wadi, kadiri iwezekanavyo, ni sawa na idadi ya watu inayolingana na eneo hilo.

(8)Ikiwa itahitajika, Tume hii itabadilisha majina na mipaka ya maeneobunge na wadi, na idadi, majina na mipaka ya wadi.

(9)Kwa kuzingatia ibara ya (1) (2),(3) na (4), majina na maelezo ya kina kuhusu mipaka ya maeneobunge na wadi yaliyoamuliwa na Tume yatachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali, na majina na maelezo hayo yataanza kutumika baada ya kuvunjwa kwa Bunge kwa mara ya kwanza baada ya kuchapishwa kwa maelezo hayo.

(10)Mtu anaweza kuwasilisha ombi kwa Mahakama Kuu chini ya Kifungu hiki ili uamuzi uliofanywa na Tume ukaguliwe.

(11)Ombi la kukaguliwa kwa uamuzi uliofanywa chini ya Kifungu hiki litawasilishwa ndani ya siku thelathini baada ya uchapishaji wa uamuzi huo katika Gazeti Rasmi la Serikali na litasikizwa na uamuzi kutolewa ndani ya miezi mitatu kuanzia siku ya kuwasilishwa kwa ombi hilo.

(12)Kwa madhumuni ya Kifungu hiki, “idadi ya watu inayolingana na eneo” inamaanisha idadi inayopatikana baada ya kugawa ifaavyo, idadi ya watu wanaoishi nchini Kenya kwa idadi ya maeneobunge au wadi ambazo Kenya imegawanywa kwayo chini ya Kifungu hiki.

Isome ndani ya Sura ya Saba →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho