Mahitaji ya kimsingi kwa vyama vya kisiasa
(1)Kila chama cha kisiasa—
(a)kitakuwa na sura ya kitaifa kama inavyoagizwa na Sheria ya Bunge;
(b)kitakuwa na idara ya uongozi iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia;
(c)kitadumisha na kukuza umoja wa kitaifa;
(d)kitazingatia kanuni za kidemokrasia za utawala bora, kitakuza na kuendeleza demokrasia kupitia kwa uchaguzi wa mara kwa mara, wenye haki na huru katika chama;
(e)kitaheshimu haki za kila mtu kushiriki katika mchakato wa kisiasa, ikijumuisha vikundi vya watu walio wachache na wale waliotengwa;
(f)kitaheshimu na kukuza haki za binadamu na uhuru wa kimsingi, na usawa wa kijinsia na usawazishaji;
(g)kitakuza malengo na kanuni za Katiba hii na utawala wa sheria; na
(h)kitazingatia kanuni za maadili kwa vyama vya kisiasa.
(2)Chama cha kisiasa—
(a)hakitabuniwa kwenye misingi ya kidini, lugha, taifa, kabila, jinsia au eneo au kujihusisha katika kampeni za kusambaza chuki kwenye misingi kama hiyo iliyotajwa;
(b)hakitajihusisha katika au kuchochea ghasia kwa kuwatisha wanachama wake, wafuasi, wapinzani au mtu mwingine yeyote;
(c)hakitaanzisha au kudumisha vikosi vya jeshi la wanamgambo, makundi haramu au mashirika mengine kama hayo;
(d)hakitajihusisha katika utoaji hongo au aina zingine za ufisadi; au
(e)isipokuwa ilivyoelezwa katika Sura hii au katika Sheria ya Bunge, hakitakubali au kutumia rasilimali za umma ili kuimarisha maslahi ya chama au wagombeaji wake katika uchaguzi.