Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nane · Mabunge

Kifungu cha 94

Kif.94

Jukumu la Mabunge

(1)Mamlaka ya utungaji wa sheria ya Jamhuri yametolewa na wananchi, na katika kiwango cha kitaifa, yamekabidhiwa kwa Bunge, na yanatekelezwa na Bunge.

(2)Bunge linadhihirisha utofauti wa taifa, linawakilisha matakwa ya wananchi, na linatekeleza mamlaka yao makuu.

(3)Bunge linaweza kuangalia kikamilifu na kupitisha marekebisho katika Katiba hii, na kubadilisha mipaka ya kaunti kama inavyoelezewa katika Katiba hii;

(4)Bunge litalinda Katiba hii na kukuza utawala wa kidemokrasia katika Jamhuri hii.

(5)Hakuna mtu yeyote au shirika lolote, isipokuwa Bunge, ambalo lina mamlaka ya kutoa maagizo au masharti ambayo yana nguvu za kisheria nchini Kenya isipokuwa chini ya mamlaka yaliyotolewa na Katiba hii au kupitia kwa sheria.

(6)Sheria ya Bunge, au sheria ya kaunti, inayotoa mamlaka kwa idara yoyote ya Serikali, afisa wa Serikali, au mtu yeyote ili kutunga sheria ambayo ina nguvu za kisheria nchini Kenya, kama inavyokusudiwa katika Ibara ya (5), itaeleza bayana malengo na madhumuni ya kutolewa kwa mamlaka hayo, mipaka ya mamlaka hayo, hali na upeo wa sheria ambazo zinaweza kutungwa, na kanuni na viwango vya ubora vinavyotumika katika sheria iliyotungwa chini ya mamlaka hayo.

Isome ndani ya Sura ya Nane →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho