Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nane · Mabunge

Kifungu cha 99

Kif.99

Ustahiki au kutostahiki katika kuchaguliwa kama mbunge

(1)Isipokuwa kwa sababu za kutostahiki chini ya ibara ya (2), mtu yeyote anastahiki kuchaguliwa kama mwanachama wa Bunge la Kitaifa au Seneti ikiwa mtu huyo—

(a)amesajiliwa kama mpiga kura;

(b)anatosheleza mahitaji yoyote ya kielimu, ya kimaadili na ya uadilifu ambayo yanahitajika katika Katiba hii au katika Sheria; na

(c)ameteuliwa na chama cha kisiasa, au ni mgombeaji huru ambaye anaungwa mkono––

(i)na angalau wapiga kura elfu moja waliosajiliwa katika eneobunge, katika uchaguzi wa Bunge la Kitaifa; na

(ii)na angalau wapiga kura elfu mbili waliosajiliwa katika kaunti, katika uchaguzi wa Seneti.

(2)Mtu hastahiki kuchaguliwa kama mwanachama wa Bunge la Kitaifa au Seneti ikiwa mtu huyo—

(a)ni afisa wa Serikali au afisa wa umma, isipokuwa awe mwanachama wa Bunge la Kitaifa au Seneti;

(b)alihudumu kama afisa katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipakakatika kipindi cha miaka mitano iliyopita kabla ya tarehe ya uchaguzi;

(c)hajakuwa raia wa Kenya kwa angalau miaka kumi iliyopita kabla ya tarehe ya uchaguzi;

(d)ni mwakilishi wadi katika bunge la kaunti;

(e)hana akili timamu;

(f)amefilisika;

(g)anakabiliwa na hukumu ya kifungo cha miezi sita gerezani katika tarehe ya kusajiliwa kama mgombeaji, au katika tarehe ya uchaguzi; au

(h)amepatikana, kwa mujibu wa sheria yoyote, kutumia vibaya mamlaka ya ofisi ya Serikali au ya umma, au kwa njia yoyote kukiuka kanuni za Sura ya Sita.

(3)Mtu hazuiliwi kugombea chini ya ibara ya (2) isipokuwa tu pale ambapo uwezekano wote wa rufaa au kukaguliwa kwa kifungo au uamuzi husika umekwisha.

Kwenye kura yako ya 2027

Kifungu hiki kinahusu chaguzi hizi

Isome ndani ya Sura ya Nane →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho