Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kwanza

Mamlaka ya Wananchi na Ukuu wa Katiba Hii

Mamlaka ni ya wananchi wa Kenya, na Katiba hii ndiyo sheria kuu.

Vifungu 1–3 · vifungu 3

Kif.1

Mamlaka ya wananchi

(1)Mamlaka yote makuu ni ya wananchi wa Kenya na yanaweza kutekelezwa tu kulingana na Katiba hii.

(2)Wananchi wanaweza kutekeleza mamlaka yao kwa njia ya moja kwa moja au kupitia wawakilishi wao waliochaguliwa kidemokrasia.

(3)Mamlaka ya wananchi katika Katiba hii yamepeanwa kwa idara za Serikali, ambazo zitafanya kazi zao kulingana na Katiba hii –

(a)Bunge la Kitaifa na mabunge katika serikali za kaunti;

(b)serikali ya kitaifa na mifumo ya serikali katika kaunti; na

(c)Idara ya Mahakama na mahakama huru ya ngazi ya chini.

(4)Mamlaka makuu ya wananchi yanatekelezwa katika––

(a)Ngazi ya kitaifa; na

(b)Ngazi yakaunti.

Kif.2

Ukuu wa Katiba Hii

(1)Katiba hii ndio sheria kuu ya Jamhuri na inapaswa kufuatwa na watu wote na idara zote za Serikali katika ngazi zote mbili za serikali.

(2)Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa na mamlaka au kutumia mamlaka ya Serikali ila tu kwa njia iliyoidhinishwa chini ya Katiba hii.

(3)Uhalali au uthabiti wa Katiba hii hauwezi kupingwa na au mbele ya mahakama yoyote au idara yoyote ya Serikali.

(4)Sheria yoyote, ikijumuisha sheria ya mila na tamaduni, ambayo haiambatani na Katiba hii ni batili kwa kiwango cha ukinzani huo, na tendo lolote au kutotenda kunakokiuka Katiba hii ni batili.

(5)Sheria za kijumla za kimataifa zitakuwa sehemu ya sheria za Kenya.

(6)Mkataba au maagano yoyote ambayo yataidhinishwa na Kenya yatakuwa sehemu ya sheria za Kenya chini ya Katiba hii.

Kif.3

Kutetea Katiba Hii

(1)Kila mtu ana jukumu la kuiheshimu, kuitetea na kuilinda Katiba hii.

(2)Jaribio lolote la kubuni Serikali bila kufuata Katiba hii ni kinyume cha sheria.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho