Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Moja

Serikali ya Ugatuzi

Kaunti 47, magavana wake na mabunge ya kaunti.

Vifungu 174–200 · vifungu 27

Sehemu 1Malengo na Kanuni za Serikali ya Ugatuzi

Kif.174

Malengo ya ugatuzi

(1)Malengo ya serikali ya ugatuzi ni—

(a)kukuza utekelezaji wa mamlaka kwa njia ya kidemokrasia na kwa uwajibikaji;

(b)kukuza umoja wa kitaifa kwa kutambua utofauti ulioko;

(c)kuwapa wananchi mamlaka ya kujitawala na kuboresha ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa mamlaka ya Serikali na katika kufanya maamuzi yanayowaathiri;

(d)kutambua haki za jamii katika kusimamia masuala ya jamii hizo na katika kuboresha maendeleo yao;

(e)kulinda na kukuza maslahi na haki za watu walio wachache na jamii zilizotengwa;;

(f)Kukuza maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi, na utoaji wa huduma zilizo karibu na zinazofikiwa kwa urahisi nchini Kenya;

(g)kuhakikisha kuna ugavi wenye usawa wa rasilimali zote za kijamii na za kitaifa kote nchini;

(h)kuwezesha ugatuzi wa vitengo vya Serikali, majukumu na huduma zao kutoka jiji kuu la Kenya; na kuboresha uwajibikaji na ugavi wa mamlaka.

Kif.175

Kanuni za serikali ya ugatuzi

(1)Serikali za kaunti zilizobuniwa chini ya Katiba hii zitazingatia kanuni zifuatazo––

(a)serikali za kaunti zitazingatia kanuni za kidemokrasia na ugawaji wa mamlaka;

(b)serikali za kaunti zitakuwa na njia zinazoweza kutegemewa katika uzalishaji wa mapato ili kuziwezesha kutawala na kutoa huduma kwa njia bora; na

(c)katika uanachama wa idara wakilishi katika kila serikali ya kaunti, idadi ya wanachama wa jinsia moja haitazidi thuluthi mbili ya wanachama wote.

Sehemu 2Serikali za Kaunti

Kif.176

Serikali za kaunti

(1)Kila kaunti itakuwa na serikali yake ya kaunti, itakayokuwa na bunge la kaunti na kitengo kinachosimamia utendaji katika kaunti.

(2)Kila serikali ya kaunti itagatua majukumu yake na utoaji wa huduma zake kwa kiwango kinachowezekana na ambacho kinaleta ufanisi.

Kif.177

Uanachama katika bunge la kaunti

(1)(1) Bunge la kaunti linajumuisha—

(a)wanachama waliochaguliwa na wapiga kura waliosajiliwa katika wadi, uchaguzi huo ukifanyika siku ile ile ya uchaguzi mkuu wa wabunge, ambayo ni Jumanne ya pili ya mwezi Agosti baada ya kila miaka mitano na kila wadi ikijumuisha eneo la kuwakilishwa na mwanachama mmoja;

(b)idadi ya wabunge maalum inayohitajika ili kuhakikisha kwamba hakuna zaidi ya wabunge thuluthi mbili wa jinsia moja katika bunge hilo;

(c)idadi ya wanachama kutoka vikundi vya watu waliotengwa, wakiwemo watu wenye ulemavu na vijana, kama inavyoagizwa katika Sheria ya Bunge; na

(d)Spika, ambaye ni mwanachama aliyechaguliwa na wabunge.

(2)Wanachama wanaobainishwa katika ibara ya (1) (b) na (c) watateuliwa na vyama vya kisiasa kulingana na idadi ya viti ambavyo kila chama cha kisiasa kilipata katika uchaguzi wa kaunti hiyo chini ya ibara ya (a) kulingana na Kifungu cha 90.

(3)Kujazwa kwa viti maalum chini ya ibara ya (1) (b) kutaamuliwa baada ya kutangazwa kwa wanachama waliochaguliwa katika kila wadi.

(4)Bunge la kaunti linachaguliwa kwa muhula wa miaka mitano.

Kif.178

Spika wa bunge la kaunti

(1)Kila bunge la kaunti litakuwa na spika aliyechaguliwa na bunge la kaunti kutoka miongoni mwa watu wasio wanachama wa bunge hilo.

(2)Kikao cha bunge la kaunti kitaongozwa na––

(a)spika wa bunge hilo; au

(b)iwapo spika hayuko, mwanachama mwingine wa bunge hilo aliyechaguliwa na bunge.

(3)Bunge litatunga sheria itakayotoa mwongozo katika kuchaguliwa na kuondolewa ofisini kwa maspika wa mabunge ya kaunti.

Kif.179

Kamati za mamlaka ya utendaji katika kaunti

(1)Mamlaka ya utendaji katika kaunti yamepewa, na yatatekelezwa, na kamati za utendaji katika kaunti.

(2)Kamati ya utendaji katika kaunti inajumuisha—

(a)gavana wa kaunti na naibu gavana wa kaunti; na

(b)wanachama walioteuliwa na gavana wa kaunti, kwa idhini ya bunge la kaunti, kutoka miongoni mwa watu ambao sio wanachama wa bunge hilo.

(3)Idadi ya wanachama walioteuliwa kwa mujibu wa ibara ya (2)(b) haitazidi—

(a)thuluthi moja ya wanachama wa bunge la kaunti ikiwa bunge hilo lina chini ya wanachama thelathini; au

(b)kumi, ikiwa bunge lina wanachama thelathini au zaidi.

(4)Gavana wa kaunti na naibu gavana wa kaunti ndio afisa mkuu na naibu wa afisa mkuu wa kaunti, mtawalia.

(5)Wakati ambapo gavana wa kaunti hayupo, naibu gavana wa kaunti ndiye atakayehudumu kama gavana wa kaunti.

(6)Wanachama wa kamati ya utendaji katika kaunti wanawajibikia gavana wa kaunti katika utekelezaji wa majukumu na mamlaka yao.

(7)Ikiwa nafasi katika ofisi ya gavana itatokea, wanachama wa kamati ya utendaji katika kaunti walioteuliwa chini ya ibara ya (2) (b) hawatahudumu tena.

Kif.180

Uchaguzi wa gavana wa kaunti na naibu gavana wa kaunti

(1)Gavana wa kaunti atachaguliwa moja kwa moja na wapiga kura waliosajiliwa katika kaunti hiyo, siku ile ile ya uchaguzi mkuu wa wabunge, itakayokuwa Jumanne ya pili ya mwezi Agosti, baada ya kila miaka mitano.

(2)Lazima mtu astahiki kuchaguliwa kama mwakilishi wadi ili astahiki kuchaguliwa kama gavana wa kaunti.

(3)Ikiwa mgombea mmoja tu wa kiti cha gavana ndiye atakayeteuliwa, mtu huyu atatangazwa kuwa amechaguliwa.

(4)Ikiwa wagombea wawili au zaidi watateuliwa, uchaguzi utafanywa katika kaunti hiyo na mgombeaji atakayepata idadi kubwa zaidi ya kura ndiye atakayetangazwa kuwa amechaguliwa.

(5)Kila mgombea kiti cha gavana wa kaunti atamteua mtu mmoja ambaye anastahiki kuchaguliwa kama gavana wa kaunti kuwa mgombea kiti cha naibu gavana.

(6)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipakahaitasimamia uchaguzi tofauti wa naibu wa gavana, lakini itamtangaza mgombea aliyeteuliwa na yule mtu anayechaguliwa kama gavana wa kaunti, kuwa amechaguliwa kama naibu wa gavana .

(7)Hakuna atakayehudumu––

(a)kama gavana wa kaunti kwa zaidi ya mihula miwili; au

(b)kama naibu gavana wa kaunti kwa zaidi ya mihula miwili.

(8)Kwa madhumuni ya ibara ya (7), mtu ambaye amechukua hatamu za uongozi kama gavana wa kaunti atachukuliwa kuwa amehudumu katika muhula mzima, lakini kwa kuzingatia Kifungu cha 182 (3) (b) tu.

Kif.181

Kuondolewa kwa serikali ya kaunti

(1)Gavana wa kaunti anaweza kuondolewa ofisini kwa msingi wowote kati ya yafuatayo––

(a)ukiukaji mkubwa wa Katiba hii au sheria yoyote nyingine;

(b)ikiwa kuna sababu kuu za kuamini kuwa gavana huyo wa kaunti amefanya uhalifu chini ya sheria ya taifa au kimataifa;

(c)matumizi mabaya ya mamlaka au mwenendo mbaya zaidi ofisini; au

(d)kukosa uwezo wa kimwili au kiakili ili kutekeleza majukumu ya ofisi ya gavana wa kaunti.

(2)Bunge litatunga sheria itakayotoa taratibu za kumwondoa gavana wa kaunti ofisini, kwenye msingi wowote kati ya iliyotajwa katika ibara ya (1).

Kif.182

Nafasi katika ofisi ya gavana wa kaunti

(1)Afisi ya gavana wa kaunti itakuwa wazi ikiwa anayehudumu katika afisi hiyo—

(a)Atafariki dunia;

(b)atajiuzulu kwa kumwandikia spika wa bunge la kaunti;

(c)atawacha kutimiza mahitaji ya kustahiki ili kuchaguliwa kama gavana wa kaunti chini ya Kifungu cha 180 (2);

(d)atapatikana na hatia ambalo linaadhibiwa kwa kifungo gerezani kisichopungua miezi kumi na miwili;

(e)ataondolewa ofisini kwa mujibu wa Katiba hii.

(2)Ikiwa nafasi itatokea katika ofisi ya gavana wa kaunti, naibu gavana wa kaunti atahudumu kama gavana wa kaunti kwa muda wa muhula uliosalia wa gavana wa kaunti.

(3)Ikiwa mtu atachukua hatamu za uongozi katika ofisi ya gavana wa kaunti chini ya ibara ya (2), kwa madhumuni ya Kifungu cha 180 (7), mtu huyo atachukuliwa kuwa—

(a)amehudumu kwa muhula mzima kama gavana wa kaunti ikiwa, katika tarehe ambayo mtu huyo alianza kuhudumu, zaidi ya miaka miwili na nusu ilikuwa inasalia kabla ya tarehe ya uchaguzi utakaofuata ulioratibiwa kikawaida chini ya Kifungu cha 180 (1); au

(b)hajahudumu kwa muhula mzima kama gavana wa kaunti katika hali nyingine yoyote.

(4)Ikiwa nafasi itatokea katika ofisi ya gavana wa kaunti na katika ofisi ya naibu gavana wa kaunti, au ikiwa naibu gavana wa kaunti hawezi kuhudumu kwa muda, spika wa bunge la kaunti ndiye atakayehudumu kwa muda kama gavana wa kaunti.

(5)Ikiwa nafasi itatokea katika hali zilizobainishwa chini ya ibara ya (4), uchaguzi wa gavana wa kaunti utafanywa ndani ya siku sitini baada ya tarehe ya spika kuanza kuhudumu kama gavana wa kaunti.

(6)Mtu atakayechukua hatamu za uongozi katika ofisi ya gavana wa kaunti chini ya Kifungu hiki, isipokuwa aondolewe ofisini vinginevyo chini ya Katiba hii, mtu huyo atahudumu hadi gavana wa kaunti aliyechaguliwa upya atakapoanza kuhudumu baada ya uchaguzi utakaofuata chini ya Kifungu cha 180 (1).

Kif.183

Majukumu ya kamati za mamlaka ya utendaji katika kaunti

(1)Kamati ya utendaji katika kaunti—

(a)itatekeleza sheria za bunge la kaunti;

(b)itatekeleza, katika kaunti, sheria za kitaifa kwa kiwango kinachohitajiwa na sheria hiyo;

(c)itasimamia na kuratibu majukumu ya utawala wa kaunti na idara zake; na

(d)itatekeleza majukumu mengine yoyote yaliyotolewa na Katiba hii na sheria ya kitaifa.

(2)Kamati ya utendaji katika kaunti inaweza kuandaa sheria iliyopendekezwa ili itathminiwe na bunge la kaunti.

(3)Kamati ya utendaji katika kaunti itatoa ripoti kamili za mara kwa mara kwa bunge la kaunti kuhusu masuala yanayohusiana na kaunti.

Kif.184

Maeneo yenye miji na majiji

(1)Sheria ya Kitaifa itatoa mwongozo kuhusu utawala na usimamizi wa maeneo ya miji na majiji, na hasa—

(a)itabuni vigezo vya kuainisha maeneo kama miji na majiji,

(b)itabuni kanuni za utawala na usimamizi wa maeneo ya miji na majiji; na

(c)itatoa mwongozo kuhusu ushiriki wa umma katika utawala wa maeneo ya miji na majiji.

(2)(2) Sheria ya kitaifa inayorejelewa katika ibara ya (1) inaweza kujumuisha njia za kutambua kategoria mbalimbali za maeneo ya miji na majiji, na utawala wao.

Kif.185

Mamlaka ya utungaji sheria ya mabunge ya kaunti

(1)Mamlaka ya kutunga sheria ya kaunti yamepewa bunge la kaunti, na yatatekelezwa na bunge la kaunti.

(2)Bunge la kaunti linaweza kutunga sheria zozote muhimu, au zinazohitajika katika ufanikishaji wa utekelezaji wa majukumu yake, na utekelezaji wa mamlaka ya serikali ya kaunti kwa mujibu wa Ambatisho la Nne.

(3)Bunge la kaunti, kwa kuzingatia kanuni ya ugawaji wa mamlaka, lina uwezo wa kusimamia kamati ya utendaji katika kaunti, pamoja na idara zinginezo katika kitengo cha utendaji cha serikali ya kaunti.

(4)Bunge la kaunti linaweza kupokea na kuidhinisha mipango na sera ya-—

(a)usimamizi na utumiaji wa rasilimali za kaunti; na

(b)maendeleo na usimamizi wa miundo-msingi na taasisi za kaunti hiyo.

Sehemu 3Majukumu na Mamlaka ya Serikali za Kaunti

Kif.186

Kazi na mamlaka ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti

(1)Isipokuwa Katiba hii itoe mwongozo vinginevyo, majukumu na mamlaka ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti ni kama yalivyoelezwa katika Ambatisho la Nne.

(2)Jukumu au mamlaka yaliyotolewa kwa zaidi ya kiwango kimoja cha serikali ni jukumu au mamlaka ambayo yanaweza kutekelezwa na viwango vyote vya serikali.

(3)Jukumu au mamlaka ambayo hayajatolewa kwa kaunti na Katiba hii au sheria ya kitaifa, ni jukumu au mamlaka ya serikali ya kitaifa.

(4)Kwa uhakika zaidi, Bunge la kitaifa linaweza kuitungia Jamhuri sheria kuhusu jambo lolote.

Kif.187

Uhamisho wa kazi na mamlaka kati ya ngazi za serikali

(1)Jukumu au mamlaka ya serikali katika ngazi moja yanaweza kuhamishwa kwa serikali katika ngazi hiyo nyingine kwa makubaliano kati ya serikali hizo mbili ikiwa—

(a)mamlaka au jukumu hilo litatekelezwa vyema zaidi na serikali hiyo inayopokea jukumu au mamlaka hayo; na

(b)kuhamishwa kwa mamlaka au jukumu hakujapigwa marufuku chini ya sheria ambayo kuhamishwa huko kungetekelezwa.

(2)Ikiwa jukumu au mamlaka yatahamishwa kutoka ngazi moja ya serikali hadi nyingine—

(a)mipango itafanywa ili kuhakikisha kwamba rasilimali zinazohitajika katika utekelezaji wa mamlaka au jukumu hilo zimehamishwa; na

(b)uwajibikaji wa kikatiba katika utekelezaji wa jukumu au mamlaka utabakia na serikali iliyopewa jukumu au mamlaka hayo chini ya Ambatisho la Nne.

Sehemu 4Mipaka ya Kaunti

Kif.188

Mipaka ya kaunti

(1)Mipaka ya kaunti inaweza kubadilishwa tu kwa uamuzi––

(a)uliopendekezwa na tume huru iliyobuniwa na bunge kwa lengo hilo; na

(b)uliopitishwa na––

(i)Bunge la Kitaifa, ukiungwa mkono na wabunge wasiopungua thuluthi mbili ya wanachama wa Bunge hilo; na

(ii)Seneti, ukiungwa mkono na angalau wajumbe wa kaunti wasiopungua thuluthi mbili ya wajumbe wa kaunti.

(2)Mipaka ya kaunti inaweza kubadilishwa ili kuzingatia—

(a)wingi wa watu na uongezekaji wao;

(b)miundombinu ya kiasili na ya kibinadamu;

(c)historia na tamaduni za watu hao;

(d)gharama ya usimamizi;

(e)maoni ya jamii zilizoathirika;

(f)malengo ya ugatuzi wa serikali; na

(g)mandhari ya kijiografia.

Sehemu 5Uhusiano Kati ya Serikali

Kif.189

Ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti

(1)Serikali katika ngazi yoyote—

(a)iwapo ni serikali ya kaunti, serikali hiyo itatekeleza majukumu na mamlaka yake kwa namna inayoheshimu hadhi na uadilifu wa kitaasisi katika ngazi hiyo ya serikali, na kwa namna inayoheshimu hadhi ya kikatiba na taasisi za serikali katika ngazi hiyo nyingine ya serikali;

(b)itasaidia, itashirikiana na kushauriana na serikali katika ngazi hiyo nyingine, na ifaavyo, itatekeleza sheria za serikali iliyo katika ngazi hiyo nyingine; na

(c)itashauriana na serikali katika kiwango hicho kingine kwa madhumuni ya kubadilishana mawazo, kuratibia sera na utawala, na kuboresha uwezo wa kutekeleza majukumu.

(2)Serikali katika ngazi zote, na serikali tofauti katika ngazi ya kaunti, zitashirikiana katika kutekeleza majukumu na mamlaka yao, na kwa lengo hilo, zinaweza kubuni kamati na mamlaka ya pamoja.

(3)Katika mzozo wowote kati ya serikali, serikali hizo zitachukua hatua zote iwezekanavyo ili kutatua mzozo huo, ikijumuisha taratibu zilizotolewa chini ya sheria ya kitaifa.

(4)Sheria ya kitaifa itatoa taratibu za kutatua mizozo kati ya serikali kwa mbinu mbadala za kutatua mizozo zikiwemo kushauriana na upatanishi.

Kif.190

Usaidizi kwa serikali za kaunti

(1)Bunge litatunga sheria ili kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zina usaidizi wa kutosha ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yao.

(2)Serikali za kaunti zitaendesha mifumo ya usimamizi wa fedha inayoafikiana na matakwa ya sheria ya kitaifa.

(3)Bunge litatunga sheria itakayoruhusu serikali ya kitaifa kuingilia kati ikiwa serikali ya kaunti—

(a)imeshindwa kutekeleza majukumu yake; au

(b)haiendeshi mfumo wa usimamizi wa fedha unaoambatana na matakwa ya sheria ya kitaifa.

(4)Sheria inayorejelewa katika ibara ya (3) inaweza, hasa, kuipa serikali ya kitaifa mamlaka ya-—

(a)kuchukua hatua mwafaka ili kuhakikisha kwamba majukumu ya serikali ya kaunti yanatekelezwa na kwamba serikali hiyo inaendesha mfumo wa usimamizi wa fedha unaoafikia mahitaji yaliyotolewa; na

(b)kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu husika ikiwa itahitajika.

(5)Sheria inayorejelewa chini ya ibara ya (3)—

(a)itahitaji notisi kutolewa kwa serikali ya kaunti kuhusu hatua zozote ambazo serikali ya kitaifa inanuia kuchukua;

(b)itaruhusu serikali ya kitaifa kuchukua tu hatua ambazo ni muhimu;

(c)itahitaji serikali ya kitaifa kuchukua hatua ambazo zitaisaidia serikali ya kaunti kurejelea kikamilifu utekelezaji wa majukumu yake serikali hiyo inapoingilia kati; na

(d)itatoa mchakato ambao Seneti inaweza kutumia ili kukomesha uingiliaji kati wa serikali ya kitaifa.

Kif.191

Mgongano wa sheria

(1)Kifungu hiki kinahusu mgongano kati ya sheria za kitaifa na zile za kaunti, katika masuala ambayo viwango vyote viwili vya serikali vina mamlaka au majukumu kuyahusu.

(2)Sheria ya kitaifa itatawala juu ya sheria ya kaunti ikiwa—

(a)sheria za kitaifa inatumika kwa usawa kote nchini Kenya na masharti mengine yaliyowekwa katika ibara ya (3) yametoshelezwa; au

(b)sheria ya kitaifa inalenga kudhibiti hatua zisizofaa katika kaunti, ikiwa hatua hizo—

(i)zinaweza kuwa na athari mbaya kiuchumi, kiafya au katika usalama wa Kenya au kaunti nyingine; au

(ii)zitazuia utekelezaji wa sera ya kiuchumi ya kitaifa.

(3)Masharti yanayorejelewa katika ibara ya (2) (a) ni kama yafuatayo (2) (a)––

(a)sheria ya kitaifa inatoa mwongozo kuhusu suala ambalo haliwezi kudhibitiwa kwa ufanisi na sheria zitakazotungwa katika kila kaunti;

(b)sheria ya kitaifa inatoa mwongozo kuhusu suala ambalo linahitaji usawa kote nchini ili kutekelezwa kwa ufanisi, na sheria hiyo ya kitaifa inatoa usawa huo kwa kubuni—

(i)kanuni na viwango vya ubora; au

(ii)sera za kitaifa; au

(c)sheria hiyo ya kitaifa ni muhimu katika—

(i)kudumisha usalama wa kitaifa;

(ii)kudumisha umoja wa kiuchumi;;

(iii)kulinda soko la shirikisho katika usafirishaji wa bidhaa, huduma, rasilimali na wafanyakazi;

(iv)kukuza shughuli za kiuchumi katika mipaka ya kaunti;

(v)kukuza nafasi sawa au usawa katika ufikiaji wa huduma za serikali; au

(vi)kulinda mazingira.

(4)Sheria ya kaunti zitatawala juu ya sheria ya kitaifa ikiwa hali zote zinazobainiwa katika ibara ya (2) hazitumiki.

(5)Katika kutatua mgongano kati ya sheria za viwango tofauti vya serikali, mahakama itapendelea ufasiri wa sheria ambao utazuia mgongano badala ya ufasiri ambao utapelekea mgongano.

(6)Uamuzi wa mahakama kwamba kifungu cha sheria ya kiwango kimoja cha serikali kinatawala juu ya kifungu katika sheria ya kiwango kingine cha serikali hakubatilishi kifungu cha sheria cha kiwango kile kingine, ila tu kifungu hicho hakitatekelezwa kwa kiwango ambacho hakiambatani na kifungu kilichoamuliwa kutawala.

Sehemu 6Kusimamishwa kwa Muda kwa Serikali za Kaunti

Kif.192

Kusimamishwa kwa serikali ya kaunti

(1)Rais anaweza kusimamisha serikali ya kaunti kwa muda—

(a)katika hali ya dharura inayotokana na mzozo wa kindani au vita; au;

(b)katika hali zingine maalum.

(2)Serikali ya kaunti haitasimamishwa kwa muda chini ya ibara ya (1) (b) isipokuwa tume huru imefanya uchunguzi wa madai dhidi ya serikali ya kaunti, Rais ameridhika kwamba madai hayo yamethibitishwa na Seneti imeidhinisha kusimamishwa huko.

(3)Kwa wakati ambao serikali ya kaunti imesimamishwa kwa muda chini ya Kifungu hiki, mikakati itawekwa ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya serikali ya kaunti kulingana na Sheria ya Bunge.

(4)Kwa wakati wowote, Seneti inaweza kutupilia mbali kusimamishwa huko.

(5)Kusimamishwa kwa muda chini ya Kifungu hiki hakutaendelea kwa zaidi ya kipindi cha siku tisini.

(6)Kipindi kilichotolewa chini ya ibara ya (5) kinapokamilika, uchaguzi wa serikali ya kaunti husika utafanyika.

Sehemu 7Vifungu vya Kijumla

Kif.193

Ustahiki katika kuchaguliwa kama mwakilishi wadi katika bunge la kaunti

(1)Isipokuwa kutostahiki chini ya ibara ya (2),mtu anastahiki kuchaguliwa kama mwakilishi wadi katika bunge la kaunti ikiwa mtu huyo—

(a)amesajiliwa kama mpiga kura;

(b)anatosheleza mahitaji yoyote ya kielimu, ya kimaadili na ya uadilifu ambayo yanahitajika katika Katiba hii au katika Sheria ya Bunge; na

(c)lazima awe—

(i)ameteuliwa na chama cha kisiasa; au

(ii)mgombea huru anayeungwa na angalau wapiga kura mia tano waliosajiliwa katika wadi husika.

(2)Mtu hastahiki kuchaguliwa kama mwakilishi wadi ikiwa mtu huyo—

(a)ni afisa wa Serikali au wa umma, isipokuwa mwakilishi wadi katika bunge la kaunti;

(b)amehudumu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka katika miaka mitano iliyopita kabla ya tarehe ya uchaguzi.

(c)hajakuwa raia wa Kenya kwa angalau miaka kumi iliyopita kabla ya tarehe ya uchaguzi;

(d)hana akili timamu;

(e)amefilisika;

(f)anatumikia kifungo gerezani cha miezi sita au zaidi; au

(g)amepatikana kuwa, kulingana na sheria yoyote, ametumia vibaya mamlaka ya ofisi ya umma au kuwa amekiuka Sura ya Sita.

(3)Mtu hazuiliwi kugombea chini ya ibara ya (2) isipokuwa tu pale ambapo uwezekano wote wa rufaa au kukaguliwa kwa kifungo au uamuzi husika umekwisha.

Kif.194

Kuondolewa ofisini kwa mwakilishi wadi katika bunge la kaunti

(1)Afisi ya mwakilishi wadi itakuwa wazi—

(a)ikiwa mwakilishi wadi huyo atafariki dunia;

(b)Ikiwa mwakilishi wadi huyo atakosa kuhudhuria vikao vinane vya bunge bila idhini iliyoandikwa ya spika wa bunge, na hawezi kutoa sababu za kutosheleza kuhusu kutohudhuria huko;

(c)ikiwa mwanachama huyo ameondolewa ofisini vinginevyo chini ya Katiba hii au chini ya sheria iliyotungwa chini ya Kifungu cha 80;

(d)Ikiwa mwakilishi wadi huyo atajiuzulu kwa kumwandikia spika wa bunge la kaunti;

(e)ikiwa baada ya kuchaguliwa katika bunge la kaunti––

(i)kama mwanachama wa chama cha kisiasa, mwakilishi wadi huyo atajiuzulu kutoka chama hicho, au ikiwa atachukuliwa kuwa amejiuzulu kulingana na sheria

(ii)inavyobainishwa katika ibara ya (2); au

(iii)kama mgombea huru, mwanachama huyo atajiunga na chama cha kisiasa;

(f)mwishoni mwa muhula wa bunge hilo la kaunti; au

(g)ikiwa mwakilishi wadi huyo hatastahiki kuchaguliwa kwenye misingi iliyobainiwa katika Kifungu cha 193 (2).

(2)Bunge litatunga sheria litakalotoa hali ambazo mwanachama wa chama cha kisiasa atachukuliwa kuwa amejiuzulu kutoka chama hicho, kwa madhumuni ya ibara ya (1) (e).

Kif.195

Mamlaka ya bunge la kaunti ya kuwaita mashahidi

(1)Bunge la kaunti au yoyote kati ya kamati zake, lina uwezo wa kumwita mtu yeyote mbele yake kwa madhumuni ya kutoa ushahidi au maelezo.

(2)Kwa madhumuni ya ibara ya (1), bunge la kaunti lina mamlaka sawa na Mahakama Kuu katika—

(a)kuamrisha mashahidi kuhudhuria na kuwahoji baada ya wao kula kiapo, kutoa uthibitisho au vinginevyo;

(b)kulazimisha utoaji wa hati; na

(c)Kutoa ombi la kuwahoji mashahidi walio ng’ambo.

Kif.196

Kushiriki kwa umma na mamlaka, haki maalum na kinga dhidi ya mashtaka kwa bunge la kaunti

(1)Bunge la kaunti—

(a)litaendesha shughuli zake kwa uwazi, na kufanya vikao vyake na vya kamati zake hadharani; na

(b)litawezesha ushiriki wa umma katika kutunga sheria na katika shughuli zingine za bunge hilo na za kamati zake.

(2)Bunge la kaunti halitazuia umma, au vyombo vya habari, kuhudhuria kikao chochote isipokuwa katika hali maalum ambayo spika wa bunge ameamua kwamba kuna sababu zinazotosheleza za kufanya hivyo.

(3)Bunge la kitaifa litatunga sheria itakayotoa mwongozo kuhusu mamlaka, haki maalum na kinga dhidi ya mashtaka kwa mabunge ya kaunti na wanachama wake.

Kif.197

Usawa wa kijinsia na utofauti katika bunge la kaunti

(1)Idadi ya jinsia moja ya wanachama wa bunge lolote la kaunti au wa kamati ya utendaji katika kaunti, halitazidi thuluthi mbili ya wanachama hao.

(2)Bunge litatunga sheria ili—

(a)kuhakikisha kwamba utofauti wa kijamii na wa kitamaduni unazingatiwa katika bunge la kaunti na kamati za utendaji katika kaunti; na

(b)kuweka mikakati ya kuwalinda walio wachache katika kaunti hizo.

Kif.198

Serikali ya kaunti katika kipindi cha mpito

Uchaguzi utakapofanywa ili kuunda bunge la kaunti chini ya Sura hii, kamati ya utendaji katika kaunti, ilivyoundwa mara ya mwisho, itakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu ya usimamizi hadi kamati mpya ya utendaji itakapoundwa baada ya uchaguzi.

Kif.199

Kuchapishwa kwa sheria za kaunti

(1)Sheria ya kaunti haianzi kutumika isipokuwa ichapishwe katika Gazeti Rasmi la Serikali.

(2)Sheria ya kitaifa na sheria za kaunti zinaweza kutoa masharti ya ziada kuhusu uchapishaji wa sheria za serikali ya kaunti.

Kif.200

Sheria Kuhusu Sura Hii

(1)Bunge litatunga sheria itakayotoa mwongozo katika masuala yote muhimu au yanayohitajika ili kuwezesha utekelezaji wa Sura hii.

(2)Hasa, sheria inaweza kubuniwa ili iangazie––

(a)usimamizi wa mji mkuu, majiji mengine na maeneo ya miji;

(b)kuhamishwa kwa majukumu na mamlaka kutoka ngazi moja cha serikali hadi nyingine, ikijumuisha kuhamisha uwezo wa kutunga sheria kutoka kwa serikali ya kitaifa hadi serikali za kaunti;

(c)taratibu za uchaguzi au uteuzi wa watu, na kuondolewa kwao ofisini katika serikali za kaunti, ikijumuisha ustahiki wa wapiga kura na wagombeaji;

(d)taratibu za mabunge ya kaunti na kamati za utendaji katika kaunti, ikijumuisha mwenyekiti wa mikutano na jinsi mikutano hiyo itafanywa, idadi ya watu wanaohitajika ili mkutano kufanyika na upigaji kura; na

(e)kusimamishwa kwa muda kwa mabunge ya kaunti na kamati za utendaji. Sehemu ya I—Kanuni na Taratibu Kuhusu Fedha za Umma

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho