Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Mbili

Fedha za Umma

Jinsi pesa za umma zinavyokusanywa, kugawanywa na kutumiwa.

Vifungu 201–231 · vifungu 31

Kif.201

Kanuni za fedha za umma

Kanuni zifuatazo zitaongoza maswala yote yanayohusiana na fedha za umma katika Jamhuri-—

(a)kutakuwa na uwazi na uwajibikaji, ikijumuisha kushiriki kwa umma katika maswala ya kifedha;

(b)mfumo wa fedha za umma utakuza jamii yenye usawa, na hasa—

(i)mzigo wa utozaji ushuru utashirikiwa kwa haki;

(ii)mapato yanayopatikana katika ngazi ya kitaifa yatagawanywa kwa usawa kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti; na

(iii)matumizi ya fedha yatakuza maendeleo yenye usawa nchini, ikijumuisha utoaji wa mgao maalum kwa vikundi vya watu waliotengwa au wanaotoka maeneo yaliyotengwa; na

(c)mizigo na manufaa ya matumizi ya rasilimali na ukopaji wa umma yatashirikiwa kwa usawa kati ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo;

(d)fedha za umma zitatumiwa kwa njia ya busara na yenye uwajibikaji; na

(e)usimamizi wa fedha utakuwa wenye uwajibikaji, na kuripoti kuhusu hazina ya serikali na matumizi yake kutakuwa wazi.

Kif.202

Ugavi wenye usawa wa mapato ya kitaifa

(1)mapato yanayozalishwa katika kiwango cha kitaifa yatashirikiwa kwa usawa kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti;

(2)Serikali za kaunti zinaweza kupewa mgao wa ziada kutoka kwenye sehemu ya mapato ya serikali ya kitaifa, kwa masharti au bila masharti.

Kif.203

Ugavi wenye usawa na sheria zingine za kifedha

(1)Vigezo vifuatavyo vitazingatiwa katika kutoa uamuzi kuhusu migao sawa iliyobainiwa chini ya Kifungu cha 202 na katika sheria zote za kitaifa zinazohusu serikali ya kaunti zinazotungwa kulingana na Sura hii—

(a)maslahi ya kitaifa;

(b)mgao wowote ambao lazima utolewe kwa mujibu wa deni la umma na majukumu mengine ya kitaifa;

(c)mahitaji ya serikali ya kitaifa yatakayoamuliwa kwa kutumia vigezo visivyoegemea upande wowote;

(d)hitaji la kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zina uwezo wa kutekeleza majukumu yaliyotolewa kwa serikali hizo;

(e)uwezo wa kifedha na ufanisi wa serikali za kaunti;

(f)maendeleo na mahitaji mengine ya serikali za kaunti;

(g)tofauti za kiuchumi miongoni mwa kaunti na kati ya kaunti na hitaji la kuzisawazisha;

(h)hitaji la kuchukua hatua sawazishi kwa sababu ya maeneo na vikundi vya watu wanyonge;

(i)hitaji la kuboresha uchumi katika kila kaunti na kutoa motisha ya kuboresha uwezo wa kuzalisha mapato katika kila kaunti;

(j)matamanio kuhusu mgao wa mapato ulio thabiti na unaoweza kutabirika;

(k)hitaji la wepesi katika kukabiliana na majanga na mahitaji mengine ya muda mfupi, kwenye misingi sawa ya vigezo visivyoegemea upande wowote.

(2)Katika kila mwaka wa fedha, mgao unaolingana na mapato yaliyozalishwa kitaifa ambao utatengewa serikali za kaunti hautakuwa chini ya asilimia kumi na tano ya mapato yote ambayo yalikusanywa na serikali ya kitaifa.

(3)Kiasi cha fedha zilizotajwa katika ibara ya (2) zitahesabiwa kwenye msingi wa akaunti zilizokaguliwa hivi majuzi kuhusu mapato yaliyokusanywa, kama ilivyoidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Kif.204

Hazina ya Usawazishaji

(1)Imebuniwa Hazina ya Usawazishaji ambayo itachukua asilimia ya nusu moja ya mapato yote yatakayokusanywa na serikali ya kitaifa katika kila mwaka, mapato hayo yakihesabiwa kwenye msingi wa akaunti zilizokaguliwa hivi majuzi kuhusu mapato yaliyokusanywa, kama ilivyoidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

(2)Serikali ya kitaifa itatumia Hazina ya Usawazishaji kutoa huduma za kimsingi tu ikijumuisha maji, barabara, matibabu na nguvu za umeme katika maeneo yaliyotengwa kwa kiwango kitakachoboresha huduma hizo katika maeneo hayo ili ziwe sawa na viwango vya huduma vinavyotolewa katika maeneo mengine nchini, kama iwezekanavyo.

(3)Serikali ya kitaifa inaweza kutumia Hazina ya Usawazishaji––

(a)kwa kiasi tu ambacho matumizi ya fedha za hazina hiyo yameidhinishwa tu katika Mswada wa Matumizi ya Fedha uliopitishwa na Bunge; na

(b)kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo kupitia kwa ruzuku zilizo na kwa kaunti ambazo zina jamii zilizotengwa.

(4)Ushauri wa Tume ya Ugavi wa Mapato utatafutwa na mapendekezo yake kuzingatiwa kabla ya Bunge kupitisha Mswada wowote unaoidhinisha matumizi ya fedha kutoka kwenye Hazina ya Usawazishaji.

(5)Fedha zozote katika Hazina ya Usawazishaji ambazo hazitakuwa zimetumiwa kufikia mwisho wa mwaka wa kifedha, zitasalia katika Hazina hiyo kwa matumizi kulingana na ibara ya (2) na (3) katika mwaka wa fedha utakaofuata.

(6)Kutekelezwa kwa Kifungu hiki kutamalizika miaka ishirini baada ya tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii, lakini kwa kuzingatia ibara ya (7).

(7)Bunge linaweza kupitisha sheria itakayositisha utekelezaji wa ibara ya (6) kwa kipindi cha ziada cha miaka iliyowekwa, lakini kwa kuzingatia ibara ya (8).

(8)Sheria chini ya ibara ya (7) itaungwa na zaidi ya nusu ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa, na zaidi ya nusu ya wajumbe wote wa kaunti katika Seneti.

(9)Fedha hazitaondolewa katika Hazina ya Usawazishaji isipokuwa Msimamizi wa Bajeti awe ameidhinisha kuondolewa huko.

Kif.205

Mashauriano kuhusu sheria za kifedha zinazoathiri kaunti

(1)Wakati ambao Mswada unaojumuisha miongozo kuhusu ugavi wa mapato, au suala lolote la kifedha linalohusu serikali za kaunti utakapochapishwa, Tume ya Ugavi wa Mapato itachunguza miongozo hiyo na kutoa mapendekezo kwa Bunge la Kitaifa na Seneti.

(2)Mapendekezo yoyote ya Tume hii yatawasilishwa Bungeni, na kila Kitengo cha Bunge kitazingatia mapendekezo hayo kabla ya kupigia Mswada huo kura.

Sehemu 2Hazina Zinginezo za Umma

Kif.206

Hazina ya jumla na hazina zingine za umma

(1)Hazina Jumuishi imebuniwa, ambayo itahifadhi fedha zilizozalishwa au kupokewa na, au kwa niaba ya serikali ya kitaifa, isipokuwa fedha ambazo—

(a)zimetengwa kutoka kwa Hazina hiyo kwa sababu maalum zilizotolewa na Sheria ya Bunge, na ambazo zitawekwa katika hazina nyingine ya umma iliyobuniwa kwa lengo maalum; au

(b)zinaweza, chini ya Sheria ya Bunge, kuhifadhiwa na kitengo cha Serikali kilichozipokea kwa lengo la kugharamia mahitaji ya kitengo hicho.

(2)Fedha zinaweza kuondolewa kutoka kwenye Hazina Jumuishi tu—

(a)kulingana na kuidhinishwa kwa matumizi yake kupitia kwa Sheria ya Bunge;

(b)kulingana na Kifungu cha 222 au 223; au

(c)kama malipo kutoka kwa Hazina hiyo kama ilivyoidhinishwa na Katiba hii au na Sheria ya Bunge.

(3)Fedha hazitaondolewa kwenye hazina nyingine yoyote ya fedha za umma kando na Hazina Jumuishi, isipokuwa kuondolewa kwa fedha hizo kumeidhinishwa na Sheria ya Bunge.

(4)Fedha hazitaondolewa kwenye Hazina Jumuishi isipokuwa Msimamizi wa Bajeti ameidhinisha kuondolewa huko.

Kif.207

Hazina za Mapato za serikali za kaunti

(1)Hazina ya Mapato ya kila serikali ya kaunti imeundwa. Hazina hii itapokea fedha zote zilizozalishwa au kupokelewa na, au kwa niaba ya serikali ya kaunti, isipokuwa fedha ambazo kwa sababu maalum zimetengwa na Sheria ya Bunge.

(2)Fedha zinaweza kutolewa kutoka kwenye Hazina ya Mapato ya serikali ya kaunti—

(a)kama malipo yanayotolewa kwenye Hazina ya Mapato na ambayo yameidhinishwa na Sheria ya Bunge au sheria ya kaunti; au

(b)kama ilivyoidhinishwa na sheria ya matumizi ya fedha katika kaunti hiyo.

(3)Fedha hazitatolewa kwenye Hazina ya Mapato isipokuwa Msimamizi wa Bajeti aidhinishe kutolewa huko.

(4)Sheria ya Bunge inaweza—

(a)kutoa idhini ya ziada ya kutolewa kwa fedha kutoka kwenye Hazina ya Mapato ya serikali ya kaunti; na

(b)kutoa mwongozo kuhusu kubuniwa kwa hazina zinginezo katika kaunti, na usimamizi wa hazina hizo.

Kif.208

Hazina ya Dharura

(1)Hazina ya Dharura imebuniwa na usimamizi wake utakuwa kulingana na Sheria ya Bunge.

(2)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu kutolewa kwa fedha kutoka kwenye Hazina ya Dharura ikiwa waziri anayehusikana na fedha ataridhika kwamba kuna hitaji la dharura na ambalo halikutarajiwa, ambalo halipo chini ya mamlaka yoyote.

Sehemu 3Deni la Umma na Mamlaka ya Kuongeza Mapato

Kif.209

Mamlaka ya kutoza ushuru na malipo mengine

(1)Serikali ya kitaifa tu ndio inayoweza kutoza—

(a)kodi ya mapato;

(b)kodi katika uuzaji wa bidhaa na huduma;

(c)ushuru wa forodha na kodi zingine zinazotozwa katika bidhaa zinazoingizwa nchini na kuuzwa nje ya nchi; na

(d)ushuru wa bidhaa zilizotengenezwa.

(2)Sheria ya Bunge inaweza kuipa mamlaka serikali ya kitaifa kutoza ushuru au kodi nyingine yoyote, isipokuwa kodi iliyotajwa katika ibara ya (3) (a) au (b).

(3)Kaunti inaweza kutoza—

(a)kodi katika umiliki wa ardhi;

(b)makodi ya burudani; na

(c)kodi nyingine yoyote ambayo imeruhusiwa na Sheria ya Bunge kutoza.

(4)Serikali ya kitaifa na serikali za kaunti zinaweza kutoza malipo kwa huduma zinazotolewa.

(5)Mamlaka ya utozaji ushuru na mengine ya kuzalisha mapato ya kaunti hayatatekelezwa kwa njia ambayo inaathirisha sera za kiuchumi za kitaifa, shughuli za kiuchumi katika mipaka ya kaunti au usafirishaji wa bidhaa, huduma, rasilimali au wafanyakazi kote nchini.

Kif.210

Kutoza ushuru

(1)Hakuna kodi yoyote au ada ya leseni itakayotozwa, kuondolewa au kubadilishwa isipokuwa kulingana na sheria.

(2)Ikiwa sheria itaruhusu kuondolewa kwa ushuru au ada ya leseni—

(a)rekodi iliyowekwa wazi kwa umma kuhusu kuondolewa kwa kodi, pamoja na sababu za kuondolewa huko itadumishwa; na

(b)kila kuondolewa kwa kodi, na sababu zake, kutaripotiwa kwa Mkaguzi Mkuu.

(3)Hakuna sheria yoyote ambayo itamtenga au kumwondoa afisa wa Serikali katika ulipaji wa ushuru kwa sababu za—

(a)ofisi ambayo afisa huyo wa Serikali anahudumu; au

(b)hali ya kazi ya afisa huyo wa Serikali.

Kif.211

Ukopaji wa serikali ya kitaifa

(1)Kupitia kwa sheria, Bunge linaweza—

(a)kutoa masharti ambayo yanapaswa kutimizwa na serikali ya kitaifa inapokopa; na

(b)kulazimisha mahitaji ya kuripoti.

(2)Katika muda wa siku saba baada ya Kitengo chochote cha Bunge kutoa ombi kwa uamuzi, Waziri anayehusikana na fedha atawasilisha maelezo kuhusu mkopo au udhamini wowote mbele ya kamati husika, ikijumuisha maelezo yote yanayohitajika ili kuonyesha—

(a)kiwango cha deni lote kwa kuonyesha kiasi hasa kilichokopwa na kiasi jumla cha riba;

(b)mkopo huo ulivyotumiwa au utakavyotumiwa;

(c)mikakati iliyowekwa ili kuulipa mkopo huo; na

(d)hatua zilizochukuliwa katika kulipa mkopo huo.

Kif.212

Ukopaji wa kaunti

(1)Serikali ya kaunti inaweza kukopa tu—

(a)ikiwa serikali ya kitaifa itadhamini mkopo huo; na

(b)kwa idhini ya bunge la kaunti.

Kif.213

Udhamini wa mikopo ya serikali ya kitaifa

(1)Sheria ya Bunge itaweka kanuni na masharti ambayo kwayo serikali ya kitaifa inaweza kudhamini mikopo.

(2)Katika muda wa miezi miwili baada ya kukamilika kwa kila mwaka wa fedha, serikali ya kitaifa itachapisha ripoti itakayoonyesha udhamini wote uliotolewa katika mwaka huo.

Kif.214

Deni la umma

(1)Deni la umma ni deni linalolipwa kutoka kwenye Hazina Jumuishi, lakini Sheria ya Bunge inaweza kutoa mwongozo kuhusu kulipwa kwa sehemu ya deni hilo kupitia kwa hazina zingine za umma.

(2)Kwa madhumuni ya kifungu hiki, “deni la umma” linamaanisha madeni yote yanayohusisha mikopo iliyokopwa au kudhaminiwa na amana iliyotolewa au kudhaminiwa na serikali ya kitaifa.

Sehemu 4Ugavi wa Mapato

Kif.215

Tume ya Ugavi wa Mapato

(1)Tume ya Ugavi wa Mapato imebuniwa.

(2)Tume hii itajumuisha watu wafuatao watakaoteuliwa na Rais—

(a)mwenyekiti, atakayeteuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa;

(b)watu wawili watakaoteuliwa na vyama vya kisiasa vinavyowakilishwa katika Bunge la Kitaifa kulingana na idadi ya wabunge katika vyama hivyo walio bungeni;

(c)watu watano watakaoteuliwa na vyama vya kisiasa vinavyowakilishwa katika seneti kulingana na idadi ya maseneta wa vyama hivyo walio katika Seneti; na

(d)Katibu Mkuu katika Wizara inayosimamia fedha.

(3)Watu watakaoteuliwa kwa mujibu wa ibara ya (2) hawatakuwa wanachama wa Bunge.

(4)Ili kuhitimu kuwa mwanachama wa Tume hii chini ya ibara ya (2) (a), (b) au (c), lazima mtu awe na uzoefu mpana wa kitaaluma katika masuala ya kifedha na uchumi.

Kif.216

Kazi ya Tume ya Ugavi wa Mapato

(1)Jukumu kuu la Tume ya Ugavi wa Mapato ni kutoa mapendekezo kuhusu misingi ya ugavi wa mapato yanayozalishwa na serikali ya kitaifa kwa njia yenye usawa––

(a)kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti; na

(b)miongoni mwa serikali za kaunti.

(2)Tume hiyo pia itatoa mapendekezo katika masuala mengine yanayohusiana na ufadhili wa serikali za kaunti na usimamizi wa fedha katika serikali hizi, kulingana na Katiba hii na sheria za kitaifa.

(3)Katika uandalizi wa mapendekezo, Tume hiyo itazingatia––

(a)kukuza na kuwezesha utekelezaji wa vigezo vilivyotajwa katika Kifungu cha 203 (1);

(b)kwa wakati ufaao, kufafanua na kuboresha njia za uzalishaji wa mapato za serikali ya kitaifa na serikali za kaunti; na

(c)kuhimiza uwajibikaji wa kifedha.

(4)Tume itaamua, itachapisha na kukagua mara kwa mara sera ambayo kwayo inatoa vigezo vya kutambua maeneo yaliyotengwa kwa madhumuni ya Kifungu cha 204 (2).

(5)Tume itawasilisha mapendekezo yake kwa Seneti, Bunge la Kitaifa, kitengo cha utendaji cha serikali ya kitaifa, mabunge ya kaunti na vitengo vya utendaji katika serikali za kaunti.

Kif.217

Ugavi wa mapato

(1)Mara moja baada ya kila miaka mitano, Seneti, kwa njia ya uamuzi, itaamua misingi itakayotumiwa kugawa mapato ya kitaifa ambayo hutolewa kwa serikali za kaunti kila mwaka.

(2)Katika kuamua msingi wa ugavi wa mapato chini ibara ya (1), Seneti—

(a)itazingatia vigezo katika Kifungu cha 203 (1);

(b)itaomba kupata mapendekezo ya Tume ya Ugavi wa Mapato na kuyazingatia;

(c)itashauriana na magavana wa kaunti, Waziri anayesimamia fedha na usimamizi wowote wa serikali za kaunti; na

(d)itawaalika watu, ikijumuisha mashirika ya kitaaluma ili yawasilishe maoni yao kuhusu suala hilo.

(3)Katika muda wa siku kumi baada ya Seneti kuidhinisha uamuzi chini ya ibara ya (1), Spika wa Seneti atawasilisha uamuzi huo kwa Spika wa Bunge la Kitaifa.

(4)Katika muda wa siku sitini baada ya uamuzi wa Seneti kuwasilishwa kama inavyorejelewa katika ibara ya (3), Bunge la Kitaifa linaweza kutathmini uamuzi huo, na kuupigia kura ili kuuidhinisha kwa marekebisho au bila marekebisho, au linaweza kuukataa.

(5)Ikiwa Bunge la Kitaifa––

(a)halitapiga kura kuhusu uamuzi huo ndani ya siku sitini, uamuzi huo utachukuliwa kuwa umeidhinishwa na Bunge la Kitaifa bila marekebisho; au

(b)litapiga kura kuhusu uamuzi huo, uamuzi huo utakuwa––

(i)umerekebishwa ikiwa angalau thuluthi mbili ya wabunge itapiga kura ya uungaji mkono wa marekebisho hayo;

(ii)umekataliwa ikiwa idadi isiyopungua thuluthi mbili ya wabunge watapiga kura kuukataa, bila kujalisha kwamba umerekebishwa kwanza na Bunge la Kitaifa; au

(iii)umeidhinishwa, katika hali nyingine yoyote.

(6)Ikiwa Bunge la Kitaifa litaidhinisha uamuzi uliorekebishwa, au kuukataa uamuzi huo, Seneti, kwa uchaguzi wake, linaweza––

(a)kupitisha uamuzi mpya chini ya ibara ya (1), na katika hali hii, miongozo katika ibara ya (4) na (5) itatumiwa upya; au

(b)kuomba kwamba suala hilo liwasilishwe mbele ya kamati ya pamoja ya Vitengo vyote viwili vya Bunge kwa madhumuni ya upatanisho chini ya Kifungu cha 113, kitakachotumiwa kwa kuzingatia mabadiliko yatakayohitajika.

(7)Uamuzi chini ya Kifungu hiki utakaokuwa umeidhinishwa chini ya ibara ya (5) utatekelezwa hadi uamuzi ufuatao utakapoidhinishwa.

(8)Licha ya ibara ya (1), Seneti, kwa uamuzi ulioungwa mkono na wanachama wasiopungua thuluthi mbili, inaweza kurekebisha uamuzi kwa wakati wowote baada ya kuidhinishwa kwake.

(9)Ibara ya (2) hadi (8), kwa kuzingatia mabadiliko yanayohitajika, zitatumika katika uamuzi uliotolewa chini ya ibara ya (8).

Kif.218

Miswada ya Ugavi wa Mapato ya Kila Mwaka

(1)Katika muda wa angalau miezi miwili baada ya kukamilika kwa kila mwaka wa kifedha, yafuatayo yatawasilishwa bungeni––

(a)Mswada Kuhusu Ugavi wa Mapato, ambao utagawa mapato yaliyozalishwa na serikali ya kitaifa kati ya viwango vya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kwa mujibu wa Katiba hii; na

(b)Mswada wa Kutenga Mapato kwa Serikali za Kaunti, ambao utagawa mapato yaliyotengwa kwa serikali za kaunti katika kila kaunti, kwenye misingi itakayoamuliwa kulingana na uamuzi unaotekelezwa chini ya Kifungu cha 217.

(2)Kila Mswada unaohitajika chini ya ibara ya (2) utaambatanishwa na hati itakayoweka wazi––

(a)maelezo kuhusu mgao wa mapato kama ilivyopendekezwa na Mswada;

(b)tathmini ya Mswada kulingana na vigezo vilivyotajwa katika Kifungu cha 203 (1); na

(c)muhtasari wa tofauti zozote muhimu dhidi ya mapendekezo ya Tume ya Ugavi wa Mapato, na maelezo kwa kila tofauti iliyopo.

Kif.219

Uhamishaji wa ugavi wenye usawa

Mgao wa kaunti wa mapato yaliyozalishwa na serikali ya kitaifa utahamishiwa kaunti bila kucheleweshwa pasipo sababu na bila kupunguzwa, isipokuwa uhamishaji huo unapositishwa chini ya Kifungu cha 225.

Sehemu 5Bajeti na Matumizi

Kif.220

Muundo, yaliyomo na wakati wa bajeti

(1)Bajeti za serikali ya kitaifa na serikali za kaunti zitajumuisha—

(a)makadirio ya mapato na matumizi, zikitofautisha matumizi ya kawaida na yale ya kimaendeleo;

(b)mapendekezo kuhusu jinsi upungufu wowote wa kifedha unaotarajiwa katika kipindi ambacho bajeti hizo zitatumika utashughulikiwa; na

(c)mapendekezo kuhusu kukopa na madeni yoyote ya umma ambayo yataongeza deni la umma katika mwaka utakaofuata

(2)Sheria za kitaifa zitatoa mwongozo kuhusu—

(a)muundo wa mipango ya maendeleo na bajeti za kaunti;

(b)wakati ambao mipango na bajeti za serikali za kaunti zitawasilishwa katika mabunge ya kaunti; na

(c)njia na namna ya mashauriano kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti katika mchakato wa kuandaa mipango na bajeti.

Kif.221

Mswada wa makadirio ya bajeti na Matumizi ya Mwaka

(1)Kwa kipindi kisichopungua miezi miwili kabla ya kukamilika kwa kila mwaka wa kifedha, Waziri anayehusika na fedha atawasilisha mbele ya Bunge la Kitaifa makadirio ya mapato na matumizi ya serikali ya kitaifa ya mwaka ufuatao wa kifedha.

(2)Makadirio yaliyotajwa katika ibara ya (1)––

(a)yatajumuisha makadirio ya matumizi kutoka kwenye Hazina ya Usawazishaji; na

(b)yatakuwa kwa muundo, na kwa mujibu wa utaratibu utakaotolewa na Sheria ya Bunge.

(3)Bunge la Kitaifa litazingatia makadirio yaliyowasilishwa chini ya ibara ya (1) pamoja na makadirio yaliyowasilishwa na Tume ya Huduma za Bunge na Msajili Mkuu wa Kitengo cha Mahakama chini ya Kifungu cha 127 na 173, mtawalia.

(4)Kabla ya Bunge la Kitaifa kuzingatia makadirio ya mapato na matumizi, kamati ya Bunge itajadili na kukagua makadirio hayo na kutoa mapendekezo yake kwa Bunge.

(5)Katika kujadili na kukagua makadirio hayo, kamati itazingatia maoni ya umma na mapendekezo hayo ya umma yatazingatiwa kamati hiyo itakapowasilisha mapendekezo yake kwa Bunge la Kitaifa.

(6)Makadirio ya matumizi ya serikali ya kitaifa na makadirio ya matumizi ya Kitengo cha Mahakama na ya Bunge yatakapoidhinishwa na Bunge la Kitaifa, makadirio hayo yatajumuishwa katika Mswada wa Matumizi ya Fedha, utakaowasilishwa mbele ya Bunge la Kitaifa ili kuidhinisha kutolewa kwa fedha za matumizi zinazohitajika kutoka kwenye Hazina Jumuishi, na kwa matumizi ya fedha hizo kwa madhumuni yaliyotajwa katika Mswada huo.

(7)Mswada wa Matumizi ya Fedha uliotajwa katika ibara ya (6) hautajumuisha matumizi yanayolipiwa kutoka kwenye Hazina Jumuishi kulingana na Katiba hii au Sheria ya Bunge.

Kif.222

Matumizi kabla ya kuidhinishwa kwa bajeti ya kila mwaka

(1)Ikiwa Sheria Kuhusu Matumizi ya Fedha katika mwaka wa kifedha haijaidhinishwa na Rais, au hakuna uwezekano mkubwa wa sheria hiyo kuidhinishwa na Rais mwanzoni mwa mwaka wa kifedha, Bunge la Kitaifa linaweza kuidhinisha kutolewa kwa fedha kutoka kwenye Hazina Jumuishi.

(2)(2) Fedha zitakazotolewa chini ya ibara ya (1)—

(a)zitatumiwa kwa madhumuni ya kuendesha huduma za serikali ya kitaifa katika mwaka huo hadi wakati ambapo Sheria Kuhusu Matumizi ya Fedha itakapoidhinishwa na Rais;

(b)kwa jumla, hazitazidi nusu ya fedha zilizopendekezwa katika makadirio ya matumizi ya mwaka huo yaliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa; na

(c)zitajumuishwa kwenye Sheria Kuhusu Matumizi ya Fedha, katika vitengo tofauti vya matumizi, na katika huduma mbalimbali ambazo fedha hizo zilikusudiwa kutekeleza.

Kif.223

Matumizi ya ziada

(1)Kwa kuzingatia ibara ya (2) hadi (4), serikali ya kitaifa inaweza kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa ikiwa—

(a)kiasi kilichotengwa kwa madhumuni yoyote chini ya Sheria Kuhusu Matumizi ya Fedha hakitoshi au hitaji limetokea la matumizi ambayo hayakuwa yamekadiriwa na kuidhinishwa na Sheria hiyo; au

(b)fedha zimetolewa kutoka kwenye Hazina ya Dharura.

(2)Idhini ya Bunge kuhusu matumizi yoyote chini ya Kifungu hiki itafuatiliwa katika muda wa miezi miwili baada ya fedha kutolewa kwa mara ya kwanza, lakini kwa kuzingatia ibara ya (3).

(3)Ikiwa Bunge halitakuwa na vikao katika muda uliobainishwa katika ibara ya (2), au lina vikao lakini liende mapumzikoni kabla ya idhini kutolewa, idhini hiyo itafuatiliwa katika muda wa wiki mbili baada ya kikao chake kitakachofuata.

(4)Bunge la Kitaifa litakapokuwa limeidhinisha matumizi chini ya ibara ya (2), Mswada kuhusu matumizi ya fedha utawasilishwa ili kuidhinisha matumizi ya fedha.

(5)Katika mwaka wowote wa kifedha, serikali ya kitaifa haiwezi kutumia fedha chini ya Kifungu hiki, kwa kiasi kinachozidi asilimia kumi ya fedha zilizotengwa na Bunge kwa mwaka huo, isipokuwa Bunge liidhinishe asilimia ya juu kuliko asilimia kumi, katika hali maalum.

Kif.224

Miswada ya matumizi ya fedha za Kaunti

Kwenye msingi ya Mswada wa Ugavi wa Mapato uliopitishwa na Bunge chini ya Kifungu cha 218, kila serikali ya kaunti itaandaa na kupitisha bajeti yake ya mwaka na Mswada wa matumizi ya fedha kwa muundo, na kulingana na taratibu zilizotolewa na Sheria ya Bunge.

Sehemu 6Udhibiti wa Fedha za Umma

Kif.225

Udhibiti wa fedha

(1)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu kubuniwa kwa Hazina ya kitaifa, majukumu na uwajibikaji wa Hazina hiyo.

(2)Bunge litatunga sheria ili kuhakikisha kuwa kunausimamizi wa matumizi na uwajibikaji katika serikali zote na litaweka mikakati ili kuhakikisha kwamba usimamizi huo na uwajibikaji umetekelezwa.

(3)Sheria chini ya ibara ya (2) inaweza kumwidhinisha Waziri anayehusika na fedha kusitisha uhamishaji wa fedha kwa kitengo fulani cha Serikali au shirika lolote la umma—

(a)iwapo tu kuna ukiukaji mkubwa au ukiukaji wa mara kwa mara wa hatua zilizowekwa chini ya sheria hiyo; na

(b)kwa kuzingatia mahitaji ya ibara ya (4) hadi ya (7).

(4)Uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha chini ya ibara ya (3) hauwezi kusitisha uhamishaji wa zaidi ya asilimia hamsini ya fedha zinazopaswa kuhamishwa kwa serikali ya kaunti.

(5)Uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha, unavyobainishwa chini ya ibara ya (3)—

(a)hautasitisha kuhamishwa kwa fedha kwa zaidi ya siku sitini; na

(b)unaweza kutekelezwa mara moja, lakini unaweza kuwacha kutekelezwa kwa mtazamo wa muda uliopita isipokuwa katika muda wa siku thelathini baada ya tarehe ya uamuzi huo, Bunge liidhinishe kwa uamuzi utakaopitishwa katika ngazi zote mbili za Bunge.

(6)Bunge linaweza kuweka upya uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha, lakini kwa siku zisizozidi sitini kwa wakati mmoja.

(7)Bunge haliwezi kuidhinisha au kuweka upya uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha isipokuwa—

(a)Msimamizi wa Bajeti amewasilisha ripoti kuhusu suala hilo Bungeni; na

(b)shirika hilo la umma limepewa nafasi ya kujibu madai dhidi yake, na kujitetea mbele ya kamati husika ya bunge.

Kif.226

Akaunti na ukaguzi wa mashirika ya umma

(1)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu—

(a)kuhifadhi rekodi za kifedha na ukaguzi wa hesabu za serikali zote na mashirika mengine ya umma, na itatoa mwongozo kuhusu hatua zinginezo za kuhakikisha usimamizi wazi wa fedha; na

(b)cheo cha afisa wa uhasibu katika kila shirika la umma katika ngazi ya serikali ya kitaifa na ya kaunti.

(2)Afisa wa uhasibu wa shirika la umma la kitaifa anawajibikia Bunge la Kitaifa katika usimamizi wa fedha wa shirika hilo, na afisa wa uhasibu wa shirika la umma la kaunti anawajibikia bunge la kaunti katika usimamizi wa fedha wa shirika hilo.

(3)Kwa kuzingatia ibara ya (4), hesabu za vitengo vyote vya Serikali na viwango vyote vya serikali zitakaguliwa na Mkaguzi Mkuu.

(4)Hesabu za ofisi ya Mkaguzi Mkuu zitakagulia na mhasibu anayestahiki kitaaluma na atakayeteuliwa na Bunge la Kitaifa, na mhasibu huyo ataripoti kuhusu hesabu hizo.

(5)Ikiwa mhudumu katika ofisi ya umma, ikijumuisha ofisi ya kisiasa, ataelekeza au kuidhinisha matumizi ya fedha za umma kinyume na sheria au maagizo, mtu huyu atawajibikia hasara yoyote itakayotokana na matumizi hayo na atagharimia hasara hiyo, bila kujalisha ikiwa mtu huyo ataendelea kuhudumu katika ofisi hiyo.

Kif.227

Ununuaji wa bidhaa na huduma za umma

(1)Kitengo cha serikali au shirika lolote la umma linapotoa kandarasi za ununuzi wa bidhaa au huduma, shirika au kitengo hicho kitafanya hivyo kulingana na mfumo ambao ni wa haki, wenye usawa, uwazi, wenye ushindani na wenye bei nafuu.

(2)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu jinsi sera zinazohusiana na ununuzi na uuzaji wa mali zitavyotekelezwa na inaweza kutoa mwongozo kuhusu suala moja au masuala yote—

(a)kategoria za kupewa kipaumbele wakati wa kutoa kandarasi;

(b)ulinzi au maendeleo ya watu, kategoria za watu au vikundi vya watu ambao walinyanyaswa kwa ushindani usio wa haki au uliowabagua na kuwatenga hapo awali;

(c)adhabu dhidi ya wanakandarasi ambao utendakazi wao hautimizi viwango vilivyokubaliwa kitaaluma, makubaliano ya kimkataba au sheria; na

(d)adhabu dhidi ya watu ambao hawajalipa kodi au ushuru, au ambao wamehusika katika ufisadi au ambao wamekiuka vikubwa sheria kuhusu uajiri wa haki.

Sehemu 6Maafisa wa Kifedha na Taasisi za Kifedha

Kif.228

Msimamizi wa Bajeti

(1)Kutakuwa na Msimamizi wa Bajeti atakayependekezwa na Rais, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, kuteuliwa na Rais.

(2)Ili kustahiki kuwa Msimamizi, lazima mtu awe na ufahamu mkubwa katika masuala ya fedha za umma, au uzoefu wa muda usiopungua miaka kumi katika ukaguzi au usimamizi wa fedha za umma.

(3)Kwa kuzingatia Kifungu cha 251, Msimamizi atahudumu kwa muhula wa miaka minane na hatastahiki kuteuliwa tena.

(4)Msimamizi wa Bajeti atasimamia utekelezaji wa bajeti ya kitaifa na bajeti za serikali za kaunti kwa kuidhinisha kutolewa kwa fedha kutoka kwa hazina za umma chini ya Vifungu vya 204, 206 na 207.

(5)***Msimamizi huyo hataidhinisha kutolewa kwa fedha kutoka kwa hazina ya umma isipokuwa aridhike kuwa kutolewa huko kumeidhinishwa kisheria.

(6)Kila baada ya miezi minne, Msimamizi huyo atawasilisha mbele ya kila Kitengo cha Bunge ripoti kuhusu utekelezaji wa bajeti ya kitaifa na bajeti za serikali za kaunti.

Kif.229

Mkaguzi Mkuu wa Serikali

(1)Kutakuwa na Mkaguzi Mkuu atakayependekezwa na Rais, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, kuteuliwa na Rais.

(2)Ili kustahiki kuwa Mkaguzi Mkuu, lazima mtu awe na ufahamu mkubwa katika masuala ya fedha za umma, au uzoefu wa muda usiopungua miaka kumi katika ukaguzi au usimamizi wa fedha za umma.

(3)Kwa kuzingatia Kifungu cha 251, Mkaguzi Mkuu atahudumu kwa muhula wa miaka nane na hatastahiki kuteuliwa tena.

(4)Katika muda wa miezi sita baada ya kukamilika kwa kila mwaka wa kifedha, Mkaguzi Mkuu, kwa madhumuni ya mwaka huo wa kifedha, atakagua na kuripoti kuhusu masuala yafuatayo—

(a)hesabu za serikali ya kitaifa na serikali za kaunti;

(b)hesabu za hazina zote na mashirika ya serikali ya kitaifa na ya serikali za kaunti;

(c)hesabu za mahakama zote;

(d)hesabu za kila tume na ofisi huru zilizobuniwa chini ya Katiba hii;

(e)hesabu za Bunge la Kitaifa, Seneti na mabunge ya kaunti;

(f)hesabu za fedha za vyama vya kisiasa ambazo zinatoka katika hazina za umma.

(g)deni la umma; na

(h)hesabu za shirika lingine lolote ambalo linatakiwa kisheria kufanyiwa ukaguzi na Mkaguzi Mkuu.

(5)Mkaguzi Mkuu anaweza kukagua na kutoa ripoti kuhusu hesabu za shirika lolote linalopokea fedha kutoka kwenye hazina za umma.

(6)Ripoti ya ukaguzi itathibitisha iwapo fedha za umma zimetumiwa kwa mujibu wa sheria na kwa njia yenye ufanisi.

(7)Ripoti za ukaguzi zitawasilishwa katika Bunge au katika bunge la kaunti.

(8)Katika muda wa miezi mitatu baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi, Bunge la Kitaifa au la kaunti litazingatia na kujadili ripoti hiyo na kuchukua hatua ifaayo.

Kif.230

Tume ya Mishahara na Malipo

(1)Tume ya Mishahara na Malipo imebuniwa.

(2)Tume ya Mishahara na Malipo inajumuisha watu wafuatao watakaoteuliwa na Rais—

(a)mwenyekiti;

(b)watu walioteuliwa na mashirika yafuatayo, miongoni mwa watu ambao sio wanachama au wafanyakazi katika mashirika hayo—

(i)Tume ya Huduma za Bunge;

(ii)Tume ya Huduma za Umma;

(iii)Tume ya Huduma za Mahakama;

(iv)Tume ya Huduma kwa Walimu;

(v)Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi;

(vi)Baraza la Ulinzi; na

(vii)Seneti, kwa niaba ya serikali za kaunti;

(c)mtu mmoja aliyeteuliwa na—

(i)shirika linalowakilisha vyama vya wafanyakazi;

(ii)shirika linalowakilisha waajiri; na

(iii)baraza la pamoja la mashirika ya kitaaluma kulingana na sheria;

(d)mtu mmoja aliyeteuliwa na—

(i)Waziri anayewajibikia masuala ya fedha; na

(ii)Mwanasheria Mkuu; na

(e)mtu aliye na uzoefu katika usimamizi wa wafanyakazi katika huduma za umma, aliyeteuliwa na Waziri anayesimamia huduma za umma.

(3)Makamishna waliotajwa katika ibara ya (1) (d) na (e) hawatakuwa na uwezo wa kupiga kura.

(4)Mamlaka na majukumu ya Tume ya Mishahara na Malipo yatakuwa—

(a)kuweka viwango vya mishahara na marupurupu ya maafisa wote wa Serikali, na kukagua mishahara na marupurupu hayo; na

(b)kushauri serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kuhusu mishahara na marupurupu ya maafisa wote wengine wa serikali.

(5)Katika kutekeleza majukumu yake, Tume hiyo itazingatia kanuni zifuatazo—

(a)hitaji la kuhakikisha kuwa bili ya kijumla ya malipo kwa umma ni endelevu kifedha;

(b)hitaji la kuhakikisha kwamba huduma za umma zina uwezo wa kuwavutia na kudumisha wahudumu walio na ujuzi unaohitajika ili kutekeleza majukumu yao;

(c)hitaji la kutambua uzalishaji na utendakazi; na

(d)uwazi na usawa.

Kif.231

Benki Kuu ya Kenya

(1)Benki Kuu ya Kenya imebuniwa.

(2)Benki Kuu ya Kenya itakuwa na jukumu la kutengeneza sera ya kifedha, kukuza udhabiti wa bei,kutoa sarafu na kutekeleza majukumu mengine kama yalivyotolewa na Sheria ya Bunge.

(3)Benki Kuu ya Kenya haitakuwa chini ya uelekezi au udhibiti wa mtu au shirika lolote katika utekelezaji wa mamlaka yake na majukumu yake.

(4)Noti na sarafu zinazotolewa na Benki Kuu ya Kenya zinaweza kuwa na picha zinazoashiria Kenya au jambo lolote kuhusu Kenya, lakini hazitakuwa na picha ya mtu yeyote.

(5)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu watakaojumuishwa katika huduma, mamlaka, majukumu na utendakazi wa Benki Kuu ya Kenya.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho