(1)Ofisi ya Inspekta-Jenerali wa Huduma za Polisi za Kitaifa imebuniwa.
(2)Inspekta-Jenerali––
(a)anateuliwa na Rais kwa idhini ya Bunge; na
(b)atatekeleza uongozi huru katika Huduma za Polisi za Kitaifa na kutekeleza majukumu mengine yoyote yatakayotolewa kwa mujibu wa sheria ya kitaifa.
(3)Huduma za Polisi nchini Kenya na Huduma za Polisi wa Utawala, zitaongozwa na Naibu Inspekta-Jenerali atakayeteuliwa na Rais kulingana na mapendekezo ya Tume ya Huduma za Polisi za Kitaifa.
(4)Waziri anayehusikana na huduma za polisi anaweza kutoa agizo kisheria kwa Inspekta-Jenerali kuhusu suala lolote la sera ya Huduma za Polisi za Kitaifa; lakini hakuna mtu yeyote atakayetoa maelekezo kwa Inspekta-Jenerali kuhusiana na—
(a)uchunguzi wa hatia fulani;
(b)utekelezaji wa sheria dhidi ya mtu au watu fulani; au
(c)kuajiriwa, kutoa majukumu, kupandishwa cheo, kusimamishwa au kufutwa kazi kwa mwanachama yeyote wa Huduma za Polisi za Kitaifa.
(5)Maelekezo yoyote yatakayotolewa na Waziri anayehusikana na huduma za polisi kwa Inspekta-Jenerali chini ya ibara ya (4), au Maelekezo yoyote yatakayotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwa Inspekta-Jenerali chini ya Kifungu cha 157 (4), yatakuwa kwa njia ya maandishi.
(6)Inspekta-Jenerali atateuliwa ili kuhudumu kwa muhula mmoja wa miaka minne, na hatastahiki kuteuliwa tena.
(7)Inspekta-Jenerali anaweza kuondolewa ofisini na Rais kwenye misingi tu ya—
(a)ukiukaji mkubwa wa Katiba hii au sheria nyingine yoyote, ikijumuisha ukiukaji wa Sura ya Sita;
(b)mwenendo mbaya zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo au vinginevyo;
(c)kutokuwa na uwezo wa kimwili au kiakili wa kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo;
(d)kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo;
(e)kufilisika; au
(f)sababu yoyote nyingine yenye haki.
(8)Bunge litatunga sheria ili kuwezesha utekelezaji wa Kifungu hiki kikamilifu.