Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Saba

Vifungu vya Kijumla

Masharti ya jumla na maana ya maneno yaliyotumika katika Katiba hii.

Vifungu 258–260 · vifungu 3

Kif.258

Utekelezaji wa Katiba Hii

(1)Kila mtu ana haki ya kuwasilisha kesi mahakamani, akidai kuwa Katiba hii imekiukwa, au kuna tishio la kuikiuka.

(2)Zaidi ya mtu anayewasilisha kesi kwa maslahi yake mwenyewe, kesi mahakamani chini ya ibara ya (1) inaweza kuwasilishwa na—

(a)mtu anayewasilisha kesi kwa niaba ya mtu mwingine ambaye hawezi kuwasilisha kesi kwa jina lake mwenyewe;

(b)mtu anayewasilisha kesi kwa niaba ya, au kama mwanachama wa kikundi au tabaka la watu;

(c)mtu anayewasilisha kesi kwa manufaa ya umma; au

(d)shirika linalowasilisha kesi kwa manufaa ya mwanachama mmoja au zaidi.

Kif.259

Kufasiri Katiba Hii

(1)Katiba hii itafasiriwa kwa namna ambayo—

(a)inakuza malengo, maadili na kanuni zake;

(b)inaendeleza utawala wa sheria, haki za binadamu na uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki;

(c)inaruhusu kuendelea kwa sheria; na

(d)inachangia katika utawala bora.

(2)Ikiwa kuna mgongano kati ya matoleo ya Katiba hii katika lugha tofauti, toleo la lugha ya Kiingereza ndilo litakalotawala.

(3)Kila kifungu katika Katiba hii litafasiriwa kulingana na kanuni ya ufasiri kwamba sheria inazungumza kila mara, na kwa hivyo, kati ya masuala mengine—

(a)jukumu au mamlaka yaliyotolewa na Katiba hii kwa ofisi yanaweza kutekelezwa na mtu anayehudumu katika ofisi hiyo kulingana na hitaji;

(b)rejeleo lolote katika Katiba hii kwa Serikali au ofisi nyingine ya umma au afisa, au mtu anayehudumu katika ofisi hiyo ni rejeleo kwa mtu anayehudumu katika ofisi hiyo kwa muda au anayetekeleza majukumu ya ofisi hiyo kwa wakati wowote ule;

(c)rejeleo katika Katiba hii kwa ofisi, kitengo cha Serikali au eneo lililotajwa katika Katiba hii litasomwa kwa kuzingatia badiliko lolote rasmi linalohitajika ili liweze kutumika katika hali hizo; na

(d)rejeleo katika Katiba hii kwa ofisi au shirika, ikiwa ofisi au shirika hilo halipo tena, ni rejeleo kwa ofisi au shirika lililorithi, au ofisi au shirika sawa na lile ambalo halipo tena.

(4)Katika Katiba hii, isipokuwa pale ambapo muktadha unahitaji vinginevyo—

(a)iwapo neno au maelezo yamefafanuliwa katika Katiba hii, tofauti zozote za kisarufi au za kimatumizi ya neno linalohusiana na jingine, soma ukizingatia mabadiliko yanayotokana na muktadha; na

(b)neno “ikijumuisha” linamaanisha “ikijumuisha, lakini bila kudhibiti”.

(5)Katika kuhesabu muda uliopita kati ya matukio mawili, kwa madhumuni yoyote chini ya Katiba hii, ikiwa muda huo umeelezwa—

(a)kama siku, basi siku ambayo tukio la kwanza linatokea haitahesabiwa, na siku ambayo tukio la mwisho linaweza kutokea itajumuishwa;

(b)kama miezi, kipindi cha muda uliowekwa unaisha mwanzoni mwa siku katika mwezi husika—

(i)ambayo ina nambari sawa kama tarehe ambayo kipindi hicho kilianza, ikiwa mwezi huo una tarehe inayolingana; au

(ii)ndiyo siku ya mwisho ya mwezi huo, katika hali yoyote nyingine; au

(c)kama miaka, kipindi cha muda huo kinamalizika mwanzoni mwa tarehe ya mwaka husika inayolingana na tarehe ambayo kipindi hicho kilianza.

(6)Ikiwa muda uliowekwa katika Katiba hii kwa madhumuni yoyote ni siku sita au chini yake, Jumapili na siku za mapumziko za kitaifa hazitahesabiwa muda huo unapohesabiwa.

(7)Ikiwa katika hali zozote maalum, kipindi cha muda kilichowekwa na Katiba hii kinakamilika siku ya Jumapili au siku ya mapumziko ya kitaifa, muda huo unaongezwa hadi siku inayofuata ambayo sio Jumapili au siku ya mapumziko ya kitaifa.

(8)Ikiwa muda fulani haujawekwa na Katiba hii katika utekelezaji wa kitendo fulani, kitendo hicho kitafanywa bila kuchelewa kusio na sababu za kuridhisha, na kulingana na itakavyohitajika mara kwa mara.

(9)Ikiwa mtu yeyote au kitengo cha Serikali kina mamlaka chini ya Katiba hii ya kuongeza kipindi cha muda uliowekwa na Katiba hii, mamlaka hayo yanaweza kutekelezwa kabla au baada ya mwisho wa kipindi hicho, isipokuwa pale ambapo nia tofauti imeelezewa wazi katika kifungu kinachotoa mamlaka hayo.

(10)Isipokuwa pale ambapo Katiba hii inaelezea vinginevyo, ikiwa mtu ameondoka katika ofisi iliyobuniwa chini ya Katiba hii, ikiwa mtu huyo anastahiki, anaweza kuteuliwa tena, kuchaguliwa au vinginevyo kuteuliwa ili kuhudumu katika ofisi hiyo kulingana na Katiba hii.

(11)Ikiwa jukumu au mamlaka yaliyotolewa kwa mtu chini ya Katiba hii yanaweza kutekelezwa na mtu huyo tu kupitia kwa ushauri au pendekezo, kupitia kwa idhini ya mtu mwingine au mashauriano na mtu mwingine, jukumu hilo linaweza kufanywa au mamlaka hayo kutekelezwa kupitia tu kwa ushauri huo, pendekezo, idhini au baada ya mashauriano hayo, isipokuwa kwa kiwango ambacho Katiba hii inatoa mwongozo vinginevyo.

Kif.260

Ufasiri

Katika Katiba hii, isipokuwa muktadha uhitaji vinginevyo—

“mtu mzima” inamaanisha mtu ambaye amefikisha umri wa miaka kumi na nane;

“hatua sawazishi” inajumuisha hatua yoyote inayolenga kuondoa hali isiyo na usawa au kunyimwa kwa haki au ukiukaji wa kimfumo wa haki na uhuru wa kimsingi; “mtoto” inamaanisha mtu ambaye hajatimiza umri wa miaka kumi na nane;

“kukiuka” inajumuisha kukosa kutimiza mahitaji yaliyowekwa;

“sheria ya kaunti” inamaanisha sheria iliyotungwa na serikali ya kaunti au chini ya mamlaka yaliyotolewa na Bunge la kaunti;

“ulemavu” inajumuisha ulemavu wowote wa kimwili, kihisia, kiakili, kisaikolojia au ulemavu wa aina nyingine, hali au ugonjwa ambao, au unaochukuliwa na sekta mahususi za kijamii kuwa na athari za muda mrefu kwa uwezo wa mtu wa kutekeleza majukumu yake ya kawaida ya kila siku; “hati” inajumuisha––

(a)chapisho lolote au suala lolote lililoandikwa, kuelezewa au kunakiliwa kwenye kitu chochote kwa kutumia herufi, michoro au alama au zaidi ya mojawapo ya njia hizo ambayo inakusudiwa kutumiwa au inaweza kutumiwa kwa madhumuni ya kurekodi suala hilo; na

(b)faili za kielektroniki;

“tarehe ya kuanza kutumika” inamaanisha tarehe ambayo Katiba hii ilianza kutumika;

“kosa” inajumuisha kukataa;

“mwaka wa kifedha” inamaanisha kipindi cha miezi kumi na miwili kinachomalizika katika siku ya thelathini ya mwezi wa Juni au siku nyingine iliyotolewa na sheria ya kitaifa, lakini mwaka wa kwanza wa kifedha wa shirika lolote ni kipindi kinachoanza wakati wa kubuniwa kwa shirika hilo hadi siku ya thelathini ya Juni ifuatayo, au siku yoyote ile itakayotolewa na sheria ya kitaifa;

“Gazeti” inamaanisha Gazeti Rasmi la Serikali linalochapishwa kutokana na kibali cha serikali ya kitaifa, au gazeti lingine linalochapishwa pamoja na Gazeti Rasmi la Kenya;

“udhamini” inamaanisha ahadi kamili au ahadi yenye masharti au kujitolea kwa serikali ya kitaifa katika ulipaji kamili au kwa kiasi wa mkopo wowote wa serikali ya kaunti au wa mtu yeyote;

“afisa wa mahakama” inamaanisha msajili, naibu wa msajili, hakimu, Kadhi au afisa msimamizi wa mahakama iliyoundwa chini ya Kifungu cha 169 (1)(d); “ardhi” inajumuisha—

(a)eneo la juu la dunia na miamba iliyo chini ya eneo hili;

(b)eneo lolote la maji juu au chini ya eneo la juu la dunia;

(c)maji ya bahari katika eneo la bahari lililo kwenye mipaka ya nchi na eneo la bahari ambalo ni la kiuchumi;

(d)mali-asili zilizopo ndani au chini ya eneo la juu la dunia; na

(e)eneo la anga juu ya eneo la juu la dunia; “sheria” inajumuisha––

(a)Sheria ya Bunge, au sheria iliyotungwa chini ya mamlaka yaliyotolewa na Sheria ya Bunge; au

(b)sheria iliyotungwa na bunge la serikali ya kaunti, au chini ya mamlaka yaliyotolewa na sheria kama hiyo;

“ mkopo” inajumuisha aina yoyote ya kukopa, kukopesha au malipo ya baadaye ambayo yanaweza kulipwa na fedha kutoka kwenye hazina ya umma, au ambayo yanahitajika kulipwa au kulipwa tena, kupitia fedha zilizo kwenye hazina ya umma;

“jamii iliyotengwa” inamaanisha—

(a)jamii ambayo kutokana na idadi ndogo ya watu wake, au kwa sababu nyingineyo, imeshindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijumla za maisha ya kijamii na kiuchumi ya Kenya;

(b)jamii ya kitamaduni, ambayo kutokana na hitaji au tamanio la kuhifadhi utamaduni wake wa na kuzuia utambulisho wake kupotea, imebakia nje ya shughuli za kijumla za maisha ya kijamii na kiuchumi ya Kenya;

(c)jamii ya kiasili ambayo imekuza na kudumisha maisha na mitindo ya kitamaduni inayojikita kwenye uchumi wa shughuli za usasi na ukusanyaji; au

(d)wafugaji au jamii za wafugaji, iwe ni—

(i)wa kuhamahama; au

(ii)jamii zinazoishi mahala pamoja na ambazo, kwa sababu ya kutengwa kijiografia, hazijashiriki kikamilifu katika shughuli za kijumla za maisha ya kijamii na kiuchumi ya Kenya;

“kikundi kilichotengwa” inamaanisha kikundi cha watu ambao, kutokana na sheria au hatua za kabla, wakati wa, au baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, walikuwa wamebaguliwa katika mojawapo au zaidi ya misingi inayotajwa katika Kifungu cha 27 (4);

“sheria ya kitaifa” inamaanisha Sheria ya Bunge, au sheria inayotungwa chini ya mamlaka yaliyotolewa na Sheria ya Bunge; “mali-asili” inamaanisha vitu au hali za kimaumbile zisizo za kibinadamu, ziwe zinaweza kutumiwa tena au la, ikijumuisha-—

(a)mwanga wa jua;

(b)maji kwenye ardhi na chini ya ardhi;

(c)misitu, uanuwai wa kiasili na kinasaba; au

(d)miamba, madini, malighafi ya mafuta na kwingine ambako kawi inapatikana;

“mzee katika jamii” inamaanisha mtu ambaye amefikisha umri wa miaka sitini;

“mtu” inajumuisha kampuni, shirika au kundi la watu, liwe limefanywa kuwa shirika au ambalo sio shirika; “chama cha kisiasa” inamaanisha muungano wa watu uliobainishwa katika Sehemu ya 3 ya Sura ya Saba;

“mali” inajumuisha haki kamili au iliyotolewa ya, au inayotokana na—

(a)ardhi au vitu vya kudumu vilivyo kwenye ardhi, au kuboreshwa kwa ardhi;

(b)bidhaa au mali ya kibinafsi;

(c)uvumbuzi; au

(d)Pesa au njia tofauti zinazotumika kama pesa;

“afisa wa umma” inamaanisha—

(e)afisa yeyote wa Serikali; au

(f)mtu yeyote, mbali na afisa wa Serikali, anayehudumu katika ofisi ya umma;

(g)”ofisi ya umma” inamaanisha ofisi katika serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti au katika huduma za umma, ikiwa malipo na marupurupu ya ofisi hiyo yanalipwa moja kwa moja kutoka kwenye Hazina Jumuishi au moja kwa moja kutoka kwenye fedha zilizotengwa na Bunge.

“huduma za umma” inamaanisha jumla ya watu wote, mbali na maafisa wa Serikali, wanaotekeleza jukumu katika kitengo cha Serikali;

“Jamhuri” inamaanisha Jamhuri ya Kenya;

“Serikali” inapotumiwa kama nomino, inamaanisha mkusanyiko wa afisa, vitengo na asasi zingine zinazounda serikali ya Jamhuri chini ya Katiba hii;

“ofisi ya Serikali” inamaanisha yoyote kati ya ofisi zifuatazo–

(a)Rais;

(b)Naibu wa Rais;

(c)Waziri;

(d)Mbunge;

(e)Majaji na Mahakimu;

(f)mwanachama wa tume chini ya Sura ya Kumi na Tano;

(g)anayehudumu katika ofisi huru chini ya Sura ya Kumi na Tano;

(h)mwakilishi wadi katika bunge la kaunti, gavana au naibu wa gavana wa kaunti, au mwanachama yeyote katika kamati ya utendaji katika serikali ya kaunti;

(i)Mwanasheria Mkuu;

(j)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma;

(k)Katibu wa Baraza la Mawaziri;

(l)Katibu Mkuu;

(m)Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya;

(n)kamanda katika huduma ya Vikosi vya Ulinzi vya Kenya;

(o)Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Upelelezi ya Kitaifa;

(p)Inspekta-Jenerali, na Manaibu wa Inspekta-Jenerali wa Huduma za Polisi za Kitaifa; au

(q)ofisi ambayo imebuniwa na kupewa hadhi ya ofisi ya Serikali chini ya sheria ya kitaifa;

“afisa wa Serikali” inamaanisha mtu anayehudumu katika ofisi ya Serikali; “kitengo cha Serikali” inamaanisha tume, ofisi, shirika au asasi nyingine iliyobuniwa chini ya Katiba hii;

“maandishi” inajumuisha upigaji chapa, upigaji picha, lithografia, upigaji taipu, breli na njia yoyote nyingine inayowakilisha au kutoa maneno kwa njia inayoonekana; na “vijana” inamaanisha jumla ya watu wote katika Jamhuri ambao—

(a)wamefikia umri wa miaka kumi na nane; lakini

(b)hawajafikia umri wa miaka thelathini na mitano.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho