Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Nane

Vifungu vya Mpito na Vitakavyotumiwa Katiba Hii Inapoanza Kutekelezwa

Kuhama kutoka Katiba ya zamani hadi hii.

Vifungu 261–264 · vifungu 4

Kif.261

Sheria zitakazofuata

(1)Bunge litatunga sheria yoyote inayohitajiwa na Katiba hii kutungwa ili kushughulikia jambo fulani katika muda ulioelezwa katika Ambatisho la Tano, kuanzia tarehe ya kutekelezwa kwa Katiba hii.

(2)Licha ya ibara ya (1), Bunge la Kitaifa, kupitia kwa uamuzi utakaoungwa mkono na idadi ya kura isiyopungua thuluthi mbili ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa, linaweza kuongeza muda uliowekwa kuhusu suala lolote kama inavyoelezwa katika ibara ya (1), kwa muda usiozidi mwaka mmoja.

(3)Mamlaka ya Bunge la Kitaifa yaliyobainiwa katika ibara ya (2) yanaweza kutumika—

(a)mara moja tu kuhusiana na suala lolote; na

(b)katika hali maalum tu ambazo zitathibitishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa.

(4)Kwa madhumuni ya ibara ya (1), Mwanasheria Mkuu akishauriana na Tume ya Utekelezaji wa Katiba hii, atatayarisha na kuwasilisha Miswada husika Bungeni, kwa haraka inavyowezekana, ili kuwezesha Bunge kupitisha sheria hizo katika muda uliowekwa.

(5)Ikiwa Bunge litashindwa kupitisha sheria yoyote katika muda uliowekwa, mtu yeyote anaweza kuwasilisha ombi katika Mahakama Kuu kuhusiana na jambo hilo.

(6)Katika kuamua ombi lililowasilishwa chini ya ibara ya (6) Mahakama Kuu inaweza—

(a)kutoa amri ya tangazo kuhusu suala hilo; na

(b)Kutoa amri inayoagiza Bunge na Mwanasheria Mkuu kuchukua hatua zitakazohakikisha kwamba sheria inayohitajika imepitishwa katika muda uliowekwa katika agizo hilo, na kutoa ripoti kuhusu utekelezaji wa hatua hizo kwa Jaji Mkuu.

(7)Ikiwa Bunge litashindwa kupitisha sheria kulingana na agizo chini ya ibara ya (6) (b), Jaji Mkuu atamshauri Rais alivunje Bunge na Rais atalivunja Bunge.

(8)Ikiwa Bunge limevunjwa chini ya ibara ya (7), Bunge jipya litapitisha sheria hiyo inayohitajika katika muda uliotajwa katika Ambatisho la Tano, kuanzia tarehe ya kuanza kwa muhula wa Bunge hilo jipya.

(9)Ikiwa Bunge jipya litakosa kupitisha sheria kulingana na ibara ya (8), masharti ya ibara ya (1) hadi ya (8) yatatekelezwa upya.

Kif.262

Vifungu kuhusu muda wa mpito na yatakayofuata

Vifungu vya mpito na vitakavyotumiwa Katiba hii itakapoanza kutekelezwa, vilivyoainishwa katika Ambatisho la Sita vitaanza kutekelezwa mnamo tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

Kif.263

Tarehe ya Kutekelezwa

Katiba hii itaanza kutumika Rais atakapotangaza rasmi au baada ya muda wa siku kumi na nne kuanzia tarehe ya kuchapisha matokeo ya mwisho ya kura ya maamuzi inayoidhinisha Katiba hii katika Gazeti Rasmi la Serikali, yoyote kati ya hatua hizo mbili itakayotekelezwa kwanza.

Kif.264

Kufutiliwa mbali kwa katiba ya hapo awali

Katiba iliyokuwa ikitumika kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii itafutuliwa mbali mnamo tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, lakini kwa kuzingatia Ambatisho la Sita.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho