Katiba ya Kenya, 2010
Sura ya Pili
Jamhuri
Kenya kama jamhuri: eneo lake, lugha, alama za taifa, maadili ya kitaifa na ugatuzi.
Teritori ya Kenya
Eneo la Jamhuri ya Kenya linajumuisha nchi kavu na maji ya Taifa la Kenya katika tarehe ya kuanza kutekelezwa, na nchi yoyote kavu na yenye maji kama inavyofafanuliwa naSheria ya Bunge.
Ugatuzi na upataji huduma
(1)Eneo la Kenya limegawanywa katika kaunti zilizotajwa katika Ambatisho la Kwanza.
(2)Serikali katika ngazi za kitaifa na kaunti ni tofauti na zinategemeana na zitahusiana kwenye msingi wa mashauriano na ushirikiano.
(3)Idara ya Serikali ya kitaifa itahakikisha upatikanaji bora wa huduma zake katika sehemu zote za Jamhuri, kwa njia inayofaa na kulingana na hali ya huduma.
Lugha ya taifa, lugha rasmi na lugha zingine
(1)Lugha ya kitaifa ya Jamhuri ni Kiswahili.
(2)Lugha rasmi za Jamhuri ya Kenya ni Kiswahili na Kiingereza.
(3)Serikali––
(a)itakuza na kulinda utofauti wa lugha za wananchi wa Kenya; na
(b)itakuza ustawi na matumizi ya lugha za kiasili, Lugha ya Ishara ya Kenya, Breli na njia zingine za mawasiliano na teknolojia zinazoweza kufikiwa na watu wenye ulemavu.
Nchi na dini
Hakutakuwa na dini ya Taifa.
Nembo za kitaifa na siku za kitaifa
(1)Nembo za kitaifa za Jamhuri ni––
(a)bendera ya taifa;
(b)wimbo wa taifa;
(c)nembo ya kitaifa inayoashiria mamlaka ya uhuru wa kujitawala; na
(d)muhuri wa serikali.
(2)Nembo za kitaifa ni kama zilivyotajwa katika Ambatisho la Pili.
(3)Siku za kitaifa ni––
(a)Siku ya Madaraka, itakayoadhimishwa tarehe 1 Juni;
(b)Siku ya Mashujaa, itakayoadhimishwa tarehe 20 Oktoba; na
(c)Siku ya Jamhuri, itakayoadhimishwa tarehe 12 Desemba.
(4)Siku ya kitaifa itakuwa siku ya mapumziko kote nchini.
(5)Bunge linaweza kupitisha sheria itakayoweka siku zingine zitakazokuwa siku za kitaifa na kuelekeza jinsi siku hizo zitakavyoadhimishwa.
Maadili ya kitaifa na kanuni za utawala
(1)Maadili ya kitaifa na kanuni za utawala katika Kifungu hiki ni lazima yafuatwe na idara zote za Serikali, maafisa wote wa Serikali, maafisa wa umma na watu wote kila wakati––
(a)wanapotekeleza au kufasiri Katiba hii;
(b)wanapopitisha, tekeleza au kufasiri sheria yoyote; au
(c)wanapotunga, au kutekeleza maamuzi kuhusu sera za umma.
(2)Maadili ya kitaifa na kanuni za utawala zinajumuisha––
(a)uzalendo, umoja wa kitaifa, kushirikiana na ugatuzi wa mamlaka, utawala wa sheria, demokrasia na kushiriki kwa watu;
(b)heshima kwa binadamu, usawa, haki za jamii, kushirikishwa, haki za binadamu, kutobaguliwa na kulindwa kwa jamii za watu waliotengwa;
(c)utawala mwema, uadilifu, uwazi na uwajibikaji; na
(d)maendeleo endelevu.
Utamaduni
(1)Katiba hii inatambua utamaduni kuwa msingi wa taifa na ustaarabu wa kijumla wa taifa na watu wa Kenya.
(2)Serikali—
(a)itakuza aina zote za kujieleza kitaifa na kitamaduni kupitia fasihi, sanaa, sherehe za kitamaduni, sayansi,
(b)mawasiliano, habari, vyombo vya habari, uchapishaji, maktaba na urithi mwingine wa kitamaduni;
(c)itatambua jukumu la sayansi na teknolojia za kiasili katika maendeleo ya nchi; na
(d)itatambua haki za kiubunifu za watu wa Kenya.
(3)Bunge litatunga sheria ili—
(a)kuhakikisha kwamba jamii zinapokea fidia au mrabaha kwa kutumiwa kwa tamaduni zao na urithi wao wa kitamaduni; na
(b)kutambua na kulinda umiliki wa mbegu na mimea mbalimbali ya kiasili, hali zao tofauti za kimaumbile na matumizi yake miongoni mwa jamii za Kenya.