Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Tano

Ardhi na Mazingira

Umiliki na matumizi ya ardhi, na kulinda mazingira na maliasili.

Vifungu 60–72 · vifungu 13

Sehemu 1Ardhi

Kif.60

Kanuni za sera ya ardhi

(1)Ardhi nchini Kenya itamilikiwa, kutumiwa na kusimamiwa kwa njia ambayo ni yenye usawa, ufanisi, uzalishaji na endelevu,na kwa kuzingatia kanuni zifuatazo—

(a)uwezo sawa wa kupata ardhi;

(b)usalama wa haki za ardhi;

(c)usimamizi endelevu na wenye manufaa, wa rasilimali za ardhi;

(d)usimamizi wa ardhi kwa uwazi na kwa gharama nafuu;

(e)hifadhi na utunzaji bora wa maeneo muhimu ya kiekolojia;

(f)kuondolewa kwa ubaguzi wa kijinsia katika sheria, mila na desturi zinazohusiana na ardhi na mali iliyomo katika ardhi; na

(g)kuhimiza jamii kutatua mizozo kuhusu ardhi kupitia hatua za kijamii zinazotambuliwa na zinazoambatana na Katiba hii.

(2)Kanuni hizi zitatekelezwa kupitia kwa sera ya ardhi ya kitaifa itakayotengenezwa na kukaguliwa mara kwa mara na serikali ya kitaifa kupitia kwa sheria.

Kif.61

Mangilio wa ardhi

(1)Ardhi yote nchini Kenya inamilikiwa na wakenya wote kijumla kama taifa, kama jamii na kama watu binafsi.

(2)Ardhi yote nchini Kenya imeainishwa kama ardhi ya umma, ya jamii au ya mtu binafsi.

Kif.62

Ardhi ya umma

(1)Ardhi ya umma ni—

(a)ardhi ambayo ilikuwa inamilikiwa na serikali na ambayo haikuwa imegawanywa wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba hii, kama ilivyoelezewa na Sheria ya Bunge wakati iliyokuwa ikitumika wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba hii;

(b)ardhi inayomilikiwa, kutumiwa au ambapo idara yoyote ya Serikali inapofanyia kazi, isipokuwa ardhi ambayo idara ya Serikali imekodisha kama mkodishaji wa kibinafsi;

(c)ardhi iliyokabidhiwa Serikali kwa njia ya kuuzwa, kurudishwa au kusalimishwa;

(d)ardhi ambayo umiliki wake wa kijamii au kibinafsi hauwezi kuthibitishwa kupitia mchakato wowote wa kisheria;

(e)ardhi ambayo hakuna mrithi yeyote anayeweza kutambuliwa kupitia mchakato wowote wa kisheria;

(f)ardhi yoyote iliyo na madini au mafuta ya madini kama ilivyoelezewa kisheria;

(g)misitu ya serikali isipokuwa misitu inayotajwa katika Kifungu cha hifadhi za wanyama, chemichemi za maji, mbuga za kitaifa, hifadhi za wanyama za serikali na maeneo maalum yaliyolindwa;

(h)barabara zote kulingana na Sheria ya Bunge;

(i)mito yote, maziwa yote na sehemu zingine za maji kama ilivyoelezewa na Sheria ya Bunge;

(j)mipaka ya bahari, maeneo maalum ya kiuchumi katika bahari na ardhi iliyo chini ya bahari;

(k)Ardhi iliyo chini ya bahari lakini kwenye upande wa bahari usio kuwa wenye kina sana;

(l)Ardhi yote iliyo kati ya nyanda za juu na za chini za maji;

(m)ardhi yoyote ambayo haijaainishwa kama ya kibinafsi au ya jamii chini ya Katiba hii; na

(n)ardhi yoyote iliyotangazwa kuwa ya umma kupitia kwa Sheria ya Bunge—

(i)Iliyokuwa ikitumika katika tarehe ya kuanza kutumika kwa katiba hii; au

(ii)iliyotungwa baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa katiba hii.

(2)Ardhi ya umma itamilikiwa na serikali ya kaunti kwa niaba ya wakazi katika kaunti hiyo, na itasimamiwa kwa niaba yao na Tume ya Kitaifa ya Ardhi ikiwa imeainishwa chini ya—

(a)sehemu ya ibara ya (1) (a), (c), (d) au (e); na

(b)sehemu ya (1) (b), isipokuwa ardhi ambayo inamilikiwa au inatumiwa na idara ya Serikali, au ambapo idara ya Serikali inafanyia kazi.

(3)Ardhi ya umma iliyoainishwa chini ya sehemu ya (1) (f) hadi (m) itamilikiwa na serikali ya kitaifa kwa niaba ya Wakenya na Tume ya Kitaifa ya Ardhi itasimamia ardhi hiyo kwa niaba yao.

(4)Ardhi ya umma haitatolewa au kutumiwa isipokuwa kwa kuzingatia Sheria ya Bunge inayofafanua hali na masharti ya kutolewa au matumizi hayo.

Kif.63

Ardhi ya jamii

(1)Ardhi ya jamii itamilikiwa na jamii zinazotambuliwa kwa misingi ya kikabila, kitamaduni au mahitaji sawa ya kijamii.

(2)Ardhi ya jamii inajumuisha—

(a)ardhi iliyosajiliwa kisheria kwa jina la wawakilishi wa kikundi chini masharti ya sheria yoyote;

(b)ardhi iliyokabidhiwa jamii fulani kisheria na kupitia kwa mchakato wowote wa kisheria;

(c)ardhi nyingine yoyote itakayotangazwa na Sheria ya Bunge kuwa ardhi ya jamii ; na

(d)ardhi ambayo—

(i)inamilikiwa kwa uhalali, inasimamiwa au kutumiwa na jamii maalum kama misitu ya jamii, maeneo ya malisho ya mifugo au mahali patakatifu pa ibada;

(ii)ni ya kiasili na ardhi ambayo kiasili inamilikiwa na jamii ya wawindaji; au

(iii)inamilikiwa kisheria kama ardhi ya amana na serikali za kaunti, lakini isiyojumuisha ardhi yoyote ya umma inayomilikiwa na serikali ya kaunti kwa niaba ya wakazi wa kaunti hiyo chini ya Kifungu cha 62 (2).

(3)Ardhi yoyote ya jamii ambayo haijasajiliwa itamilikiwa na serikali za kaunit kwa niaba ya jamii hizo.

(4)Ardhi ya jamii haitatolewa au kutumiwa vinginevyo isipokuwa kulingana na sheria inayofafanua hali na viwango vya haki za kila mwanajamii kibinafsi au wanajamii wote kwa pamoja.

(5)Bunge litatunga sheria kuwezesha utekelezaji wa Kifungu hiki.

Kif.64

Ardhi ya mtu binafsi

(1)Ardhi ya kibinafsi inajumuisha —

(a)ardhi yoyote iliyosajiliwa na inayomilikiwa na mtu yeyote chini ya umiliki unaodumu maishani mwa mtu huyo;

(b)ardhi inayomilikiwa na mtu yeyote kwa kukodisha; na

(c)ardhi yoyote nyingine iliyotangazwa kuwa ya kibinafsi chini ya Sheria ya Bunge.

Kif.65

Umiliki ardhi wa watu wasiokuwa Wakenya

(1)Mtu asiyekuwa raia wa Kenya anaweza kumiliki ardhi kwa njia ya kukodisha tu, na makubaliano yoyote ya kukodisha, bila kujalisha yalivyofikiwa, hayatazidi muda wa miaka tisini na tisa.

(2)Ikiwa kifungu katika makubaliano, mkataba au hati yoyote ya aina yoyote inampa mtu asiyekuwa raia wa Kenya uwezo wa kumiliki ardhi kwa zaidi ya miaka tisini na tisa, kifungu hicho kitachukuliwa kumpa mtu huyo umiliki wa miaka tisini na tisa na wala sio zaidi.

(3)Kwa madhumuni ya Kifungu hiki—

(a)kampuni au shirika lolote litachukuliwa kama raia tu ikiwa shirika hilo linamilikiwa kikamilifu na raia mmoja au zaidi; na

(b)Ardhi inayomilikiwa kwa niaba ya mtu au watu itachukuliwa kuwa inayomilikiwa na raia wa Kenya iwapo tu manufaa yote ya umiliki huo unawaendea watu ambao ni raia wa Kenya.

(4)Bunge linaweza kutunga sheria ili kutoa mwongozo zaidi katika utekelezaji wa Kifungu hiki.

Kif.66

Usimamizi wa matumizi ya ardhi na mali

(1)Serikali inaweza kudhibiti matumizi ya ardhi yoyote au haki yoyote katika ardhi kwa madhumuni ya ulinzi, usalama wa umma, utaratibu wa umma, maadili ya umma, afya ya umma, au mpangilio wa matumizi ya ardhi.

(2)Sheria ili kuhakikisha kwamba uwekezaji katika ardhi ni kwa manufaa ya jamii na uchumi wao.

Kif.67

Tume ya Kitaifa ya Ardhi

(1)Tume ya Huduma za Polisi za Kitaifa imebuniwa.

(2)Majukumu ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi ni—

(a)kusimamia ardhi ya umma kwa niaba ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti;

(b)kupendekezea serikali ya kitaifa sera ya kitaifa kuhusu ardhi;

(c)kushauri serikali ya kitaifa kuhusu programu ya kina itakayosimamia usajili wa umiliki wa ardhi kote nchini Kenya;

(d)kufanya utafiti unaohusiana na ardhi na matumizi ya mali-asili, na kutoa mapendekezo kwa mamlaka yanayohusika;

(e)kuanzisha uchunguzi kwa hiari yake au kutokana na malalamishi, kuhusu ukiukaji wa sasa wa haki za ardhi au ukiukaji wa kihistoria, na kupendekeza suluhisho linalofaa;

(f)kuhimiza matumizi ya njia za kitamaduni zinazotumika kusuluhisha mizozo inayohusu ardhi;

(g)kutathmini ushuru unaotozwa katika ardhi na malipo katika majengo yaliyo katika eneo lolote lililoteuliwa kisheria; na

(h)kufuatilia na kuwa na jukumu la kusimamia mpangilio wa matumizi ya ardhi kote nchini.

(3)Tume ya Kitaifa ya Ardhi inaweza kutekeleza majukumu mengine yoyote yatakayotolewa na sheria ya kitaifa.

Kif.68

Sheria zinazohusu ardhi

Bunge—

(a)litarekebisha, kuunganisha na kusawazisha sheria zilizopo kuhusu ardhi;

(b)litarekebisha sheria za kisekta kuhusu matumizi ya ardhi kulingana na kanuni zilizotajwa katika Kifungu cha 60 (1); na

(c)litatunga sheria—

(i)ili kutoa mwongozo kuhusu kiwango cha juu zaidi na cha chini zaidi cha ekari za ardhi zinazoweza kumilikiwa katika ardhi ya kibinafsi;

(ii)ili kudhibiti njia ambazo ardhi yoyote inaweza kubadilishwa kutoka kwenye mfumo mmoja hadi mwingine;

(iii)ili kudhibiti utambuzi na uhifadhi wa mali ya kindoa na hasa nyumba ya kindoa wakati wa ndoa na wakati wa kuvunjwa kwa ndoa hiyo;

(iv)ili kulinda, kuhifadhi na kuwezesha ufikiaji wa ardhi yote ya umma;

(v)ili kuwezesha kuchunguzwa kwa upataji wote au uhamishaji wote wa umiliki wa ardhi ya umma ili kuthibitisha uhalali wa upataji huo;

(vi)ili kuwalinda wategemezi wa marehemu waliomiliki ardhi, ikijumuisha maslahi ya mke au mume wa marehemu ambaye anaishi kwenye ardhi hiyo; na

(vii)Ili kutoa mwongozo katika suala lingine lolote muhimu linalohusu kuwezesha utekelezaji wa vifungu vya Sura hii.

Sehemu 2Mazingira na Mali-Asili

Kif.69

Majukumu yanayohusiana na mazingira

(1)Serikali—

(a)itahakikisha matumizi, usimamizi, na uhifadhi wa mazingira na mali-asili unaoendelea na kuhakikisha usawa katika ugavi wa manufaa yanayopatikana;

(b)itafanya juhudi ili kutimiza na kudumisha kupandwa kwa miti katika angalau asilimia kumi ya ardhi ya Kenya;

(c)italinda na kukuza haki za uvumbuzi na elimu ya kiasili katika anuwai za viumbe na rasilimali za kiasili za jamii;

(d)itahimiza kushiriki kwa umma katika usimamizi, utunzaji, na uhifadhi wa mazingira;

(e)italinda rasilmali zote za kiasili na anuwai za viumbe;

(f)itaanzisha mifumo ya kutathmini athari kwa mazingira, ukaguzi wa mazingira na usimamizi wa mazingira;

(g)itaondoa michakato na shughuli ambazo zinaweza kuhatarisha mazingira; na

(h)itatumia mazingira na mali-asili kwa manufaa ya Wakenya.

(2)Kila mtu ana jukumu la kushirikiana na idara za Serikali na watu wengine ili kulinda na kuhifadhi mazingira, na kuhakikisha kuwa kuna maendeleo endelevu ya kiekolojia na ya matumizi ya rasilimali.

Kif.70

Utekelezwaji wa haki za mazingira

(1)Ikiwa mtu atadai kuwa haki ya kupata mazingira safi na yenye afya njema inavyotambuliwa na kulindwa chini ya Kifungu cha 42 imekiukwa, inakiukwa au kuna uwezekano mkubwa wa mtu huyo kunyimwa haki hiyo au haki hiyo kukiukwa, kuvunjwa au kutishiwa, mtu huyo anaweza kuwasilisha kesi mahakamani ili kupata fidia pamoja na hatua zingine za kisheria zinazopatikana katika suala hilo.

(2)Ikiwa ombi litawasilishwa chini ya sehemu ya (1), mahakama inaweza kutoa amri, au kutoa maelekezo yoyote ambayo yanafaa––

(a)ili kuzuia, kukomesha au kusitisha tendo au kosa lolote ambalo ni hatari kwa mazingira;

(b)ili kumshurutisha afisa yeyote wa umma kuchukua hatua zitakazozuia au kusitisha tendo au kosa lolote ambalo ni hatari kwa mazingira; au

(c)kutoa fidia kwa mwathiriwa yeyote aliyeathirika kutokana na ukiukaji wa haki ya kupata mazingira safi na yenye afya njema.

(3)Kwa madhumuni ya Kifungu hiki, sio lazima kwa anayewasilisha ombi kuonyesha kwamba mtu yeyote amepata hasara au kujeruhiwa.

Kif.71

Makubaliano yanayohusiana na mali-asili

(1)Lazima makubaliano yapitishwe na Bunge ikiwa––

(a)yanajumuisha utoaji wa haki au makubaliano na mtu yeyote, au kwa niaba ya mtu yeyote, ikijumuisha serikali ya kitaifa, kwa mtu mwingine, ili atumie mali-asili yoyote iliyo nchini Kenya; na

(b)Yamefikiwa katika au baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

(2)Bunge litatunga sheria itakayotoa aina za makubaliano ambazo zitakuwa chini ya upitishaji wa Bunge kulingana na sehemu ya (1).

Kif.72

Sheria zinazohusu mazingira

Bunge litatunga sheria ili kuwezesha utekelezaji wa vifungu katika Sehemu hii.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho