Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Saba

Uwakilishaji wa Watu

Jinsi unavyopiga kura: mfumo wa uchaguzi, usajili wa wapiga kura, IEBC na vyama vya siasa.

Vifungu 81–92 · vifungu 12

Sehemu 1Mfumo na Mchakato wa Uchaguzi

Kif.81

Kanuni za kijumla za mfumo wa uchaguzi

Mfumo wa uchaguzi utazingatia kanuni zifuatazo––

(a)uhuru wa raia wa kutekeleza haki zao za kisiasa chini ya sehemu ya 38;

(b)katika mashirika ya umma ambayo wanachama huchaguliwa,wanachama wa jinsia moja hawatazidi theluthi mbili;

(c)uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwa njia yenye usawa;

(d)haki ya kupiga kura kwa wote kwenye msingi wa uwakilishaji wenye usawa na usawa wa kura; na

(e)uchaguzi huru na wenye usawa, ambao ni—

(i)wa kura ya siri;

(ii)huru na usio na ghasia, vitisho, ushawishi usiofaa, au ufisadi;

(iii)unaosimamiwa na tume huru;

(iv)wenye uwazi; na

(v)unaoendeshwa kwa njia isiyo na upendeleo, yenye ufanisi, sahihi na iliyo na uwajibikaji.

Kif.82

Sheria ya uchaguzi

(1)Bunge litatunga sheria ya kutoa mwongozo katika—

(a)ugawaji wa maeneo ya upigaji kura wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kwa sababu ya uchaguzi wa wabunge katika Bunge la Kitaifa na wawakilishi wadi katika bunge za kaunti;

(b)uteuzi wa wagombea viti;

(c)usajili unaoendelea wa raia kama wapiga kura;

(d)usimamizi wenye ufanisi na udhibiti katika uchaguzi na kura za maoni, ikijumuisha uteuzi wa wagombea katika uchaguzi; na

(e)usajili unaoendelea wa raia wanaoishi nje ya Kenya kama wapiga kura, na utekelezaji unaoendelea wa haki zao za kupiga kura.

(2)Sheria inayotakiwakatika ibara ya (1) (d) itahakikisha kwamba upigaji kura katika kila uchaguzi ni—

(a)rahisi;

(b)wenye uwazi; na

(c)unazingatia mahitaji maalumu ya—

(i)watu wenye ulemavu; na

(ii)watu wengine au jamii za watu walio na mahitaji maalum.

Kif.83

Kusajiliwa kama mpiga kura

(1)Mtu anastahiki kusajiliwa kama mpiga kura katika uchaguzi au kura za maamuzi ikiwa mtu huyo—

(a)ni raia ambaye ni mtu mzima;

(b)hajatangazwa kuwa mtu mwenye akili punguani; na

(c)hajapatikana na hatia ya uchaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

(2)Raia anayestahiki kusajiliwa kama mpiga kura atasajiliwa katika kituo kimoja tu cha usajili wa kupigia kura.

(3)Mipango ya kiusimamizi katika usajili wa wapiga kura na uendeshaji wa uchaguzi, itapangwa ili kuwezesha, na haitamnyima raia yeyote anayestahiki haki ya kupiga kura au kugombea kiti.

Kif.85

Ustahiki wa kusimama kama mgombea wa kibinafsi

Mtu yeyote anastahiki kusimama kama mgombea huru katika uchaguzi, ikiwa mtu huyo––

(a)si mwanachama katika chama cha kisiasa kilichosajiliwa na hajakuwa mwanachama kwa angalau miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi; na

(b)anatimiza mahitaji ya––

(i)Kifungu cha 99 (1) (c) (i) au (ii), ikiwa ni mgombea katika uchaguzi wa wabunge katika Bunge la Kitaifa au Seneti, mtawalia; au

(ii)Kifungu cha 193 (1) (c) (ii), ikiwa ni mgombea katika uchaguzi wa wawakilishi wadi katika bunge la kaunti.

Kif.86

Upigaji kura

Katika kila uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itahakikisha kwamba—

(1)bila kujalisha njia ya upigaji kura itakayotumiwa, mfumo huo una urahisi, ni sahihi, unaoweza kuthibitishwa, ulio salama, unaowajibika na ulio na uwazi;

(2)kura zinazopigwa zinahesabiwa, zinaorodheshwa na matokeo yanatangazwa mara moja na afisa msimamizi katika kila kituo cha upigaji kura;

(3)matokeo kutoka vituo vya upigaji kura yanajumlishwa kwa uwazi na kwa usahihi na kisha kutangazwa mara moja na afisa msimamizi katika kituo cha upigaji kura; na

(4)miundo na taratibu mwafaka zimewekwa ili kuondoa ukiukaji wa kanuni na sheria za uchaguzi, ikijumuisha uhifadhi salama wa vifaa vya uchaguzi.

Kif.87

Mizozo ya uchaguzi

(1)Bunge litatunga sheria ili kuweka taratibu za kusuluhishwa kwa mizozo ya uchaguzi katika muda unaofaa.

(2)Malalamishi kuhusu uchaguzi, isipokuwa uchaguzi wa urais, yatawasilishwa ndani ya siku ishirini na nane baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kutangaza matokeo ya uchaguzi.

(3)Ufikishaji wa malalamishi unaweza kuwa wa moja kwa moja au kwa njia ya kutangazwa katika gazeti la kitaifa.

Sehemu 2Tume Huru ya Uchaguzi na Kuwekea Mipaka Maeneo ya Upigaji Kura

Kif.88

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka

(1)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Imeundwa.

(2)Mtu hastahiki kuteuliwa kama mwanachama wa Tume ikiwa mtu huyo—

(a)ndani ya miaka mitano iliyopita, amehudumu au kugombea kiti kama—

(i)mbunge katika Bunge la Kitaifa au mwakilishi wadi katika bunge la kaunti; au

(ii)mwanachama katika idara ya uongozi wa chama cha kisiasa; au

(b)anahudumu katika ofisi yoyote ya Serikali.

(3)Mwanachama wa Tume hatahudumu katika ofisi nyingine ya umma.

(4)Tume ina wajibu wa kuendesha na kusimamia kura za maamuzi na uchaguzi katika shirika lolote ambalo wanachama wake wanachaguliwa au katika ofisi chini ya Katiba hii, na uchaguzi mwingine wowote kama ilivyoagizwa katika Sheria ya Bunge, na katika—

(a)usajili unaoendelea wa raia kama wapiga kura;

(b)ukaguzi wa mara kwa mara wa sajili ya wapiga kura;

(c)uwekaji mipaka katika maeneo bunge na wadi;

(d)kudhibiti mchakato ambao vyama hutumia katika kuteua wagombea wa uchaguzi;

(e)kusuluhisha mizozo ya uchaguzi, ikijumuisha mizozo inayohusiana au kutokana na uteuzi lakini isiyohusisha malalamishi kuhusu uchaguzi na mizozo inayotokana na kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi;

(f)usajili wa wagombea wa uchaguzi;

(g)elimu kwa wapiga kura;

(h)kuwezesha uchunguzi, usimamizi na tathmini ya uchaguzi;

(i)udhibiti wa kiwango cha fedha kinachoweza kutumiwa na mgombea au kwa niaba yake, au na chama katika uchaguzi wowote;

(j)uundaji wa kanuni za uchaguzi kwa wagombea na vyama vinavyogombea katika uchaguzi; na

(k)ufuatiliaji kuhusu ufuataji wa sheria inavyohitajika chini ya Kifungu cha 82 (1) (b) kuhusiana na uteuzi wa wagombea katika vyama.

(5)Tume itatumia mamlaka yake kutekeleza majukumu yake kulingana na Katiba hii na sheria ya kitaifa.

Kif.89

Uwekaji mipaka katika maeneo ya uchaguzi

(1)Kutakuwa na maeneo bunge mia mbili tisini kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge katika Bunge la Kitaifa kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 97 (1) (a).

(2)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itakagua majina na mipaka ya maeneo bunge kila baada ya muda usiopungua miaka nane na usiozidi miaka kumi na miwili, lakini ukaguzi wowote utakamilishwa angalau miezi kumi na miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa wabunge.

(3)Tume itakagua idadi, majina na mipaka ya wadi mara kwa mara.

(4)Ikiwa uchaguzi mkuu utafanyika ndani ya miezi kumi na miwili baada ya kukamilika kwa ukaguzi wa Tume, mipaka hiyo mipya haitazingatiwa kwa madhumuni ya uchaguzi huo.

(5)Mipaka ya kila eneobunge italinganishwa, kwa kiasi kiwezekanacho, na idadi ya wakazi katika eneo bunge hilo, lakini idadi ya wakazi katika eneobunge inaweza kuwa kubwa au ndogo kuliko idadi ya watu inayolingana na eneo hilo kwa namna ambayo imetajwa katika Ibara ya (6) ili kuzingatia—

(a)hali ya kijiografia na maeneo ya miji;

(b)jamii ya eneo lile, historia, uchumi na mahusiano ya kitamaduni; na

(c)mbinu za mawasiliano.

(6)Idadi ya wakazi katika eneobunge au wadi inaweza kuwa kubwa au ndogo zaidi ya idadi ya watu inayolingana na eneo hilo kwa kiwango kisichozidi —

(a)asilimia arobaini kwa majiji na maeneo yaliyo na idadi ya watu iliyotawanyika; na

(b)asilimia thelathini kwa sehemu nyingine.

(7)Katika kukagua mipaka ya maeneobunge na wadi, Tume-––

(a)itashauriana na wote wanaohusika; na

(b)itandelea kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba idadi ya watu katika kila eneobunge na wadi, kadiri iwezekanavyo, ni sawa na idadi ya watu inayolingana na eneo hilo.

(8)Ikiwa itahitajika, Tume hii itabadilisha majina na mipaka ya maeneobunge na wadi, na idadi, majina na mipaka ya wadi.

(9)Kwa kuzingatia ibara ya (1) (2),(3) na (4), majina na maelezo ya kina kuhusu mipaka ya maeneobunge na wadi yaliyoamuliwa na Tume yatachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali, na majina na maelezo hayo yataanza kutumika baada ya kuvunjwa kwa Bunge kwa mara ya kwanza baada ya kuchapishwa kwa maelezo hayo.

(10)Mtu anaweza kuwasilisha ombi kwa Mahakama Kuu chini ya Kifungu hiki ili uamuzi uliofanywa na Tume ukaguliwe.

(11)Ombi la kukaguliwa kwa uamuzi uliofanywa chini ya Kifungu hiki litawasilishwa ndani ya siku thelathini baada ya uchapishaji wa uamuzi huo katika Gazeti Rasmi la Serikali na litasikizwa na uamuzi kutolewa ndani ya miezi mitatu kuanzia siku ya kuwasilishwa kwa ombi hilo.

(12)Kwa madhumuni ya Kifungu hiki, “idadi ya watu inayolingana na eneo” inamaanisha idadi inayopatikana baada ya kugawa ifaavyo, idadi ya watu wanaoishi nchini Kenya kwa idadi ya maeneobunge au wadi ambazo Kenya imegawanywa kwayo chini ya Kifungu hiki.

Kif.90

Ugawaji orodha ya viti vya chama

(1)Uchaguzi wa nafasi zilizopo bungeni chini ya Kifungu cha 97 (1) (c) na 98 (1) (b), (c) na (d), na wa wawakilishi wadi chini ya Kifungu cha 177 (1) (b) na (c), utakuwa kwenye misingi ya uwakilishaji wenye usawa kwa kutumia orodha za vyama.

(2)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itawajibika katika uendeshaji na usimamizi wa uchaguzi wa nafasi zilizotolewa chini ya Ibara ya (1) na itahakikisha kwamba-—

(a)kila chama cha kisiasa kinachoshiriki katika uchaguzi mkuu kimeteua na kuwasilisha orodha ya majina ya watu wote ambao wangalichaguliwa iwapo chama hicho kingalipewa viti vyote chini ya Ibara ya (1), ndani ya muda ulioagizwa kupitia sheria ya kitaifa;

(b)isipokuwa katika nafasi zilizotolewa chini ya Kifungu cha 98 (1) (b), kila orodha ya chama ina idadi kamilifu ya wagombea wanaostahiki pamoja na watakaochukua nafasi zao, wa kiume na kike, kulingana na jinsi walivyowaorodhesha; na

(c)isipokuwa katika nafasi za bunge la kaunti, kila orodha ya chama inazingatia tofauti za kieneo na za kikabila za Wakenya.

(3)Nafasi zilizotajwa katika ibara ya (1) zitagawiwa vyama vya kisiasa kulingana na idadi ya jumla ya viti walivyoshinda wagombeaji katika chama cha kisiasa kwenye uchaguzi mkuu.

Sehemu 3Vyama vya Kisiasa

Kif.91

Mahitaji ya kimsingi kwa vyama vya kisiasa

(1)Kila chama cha kisiasa—

(a)kitakuwa na sura ya kitaifa kama inavyoagizwa na Sheria ya Bunge;

(b)kitakuwa na idara ya uongozi iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia;

(c)kitadumisha na kukuza umoja wa kitaifa;

(d)kitazingatia kanuni za kidemokrasia za utawala bora, kitakuza na kuendeleza demokrasia kupitia kwa uchaguzi wa mara kwa mara, wenye haki na huru katika chama;

(e)kitaheshimu haki za kila mtu kushiriki katika mchakato wa kisiasa, ikijumuisha vikundi vya watu walio wachache na wale waliotengwa;

(f)kitaheshimu na kukuza haki za binadamu na uhuru wa kimsingi, na usawa wa kijinsia na usawazishaji;

(g)kitakuza malengo na kanuni za Katiba hii na utawala wa sheria; na

(h)kitazingatia kanuni za maadili kwa vyama vya kisiasa.

(2)Chama cha kisiasa—

(a)hakitabuniwa kwenye misingi ya kidini, lugha, taifa, kabila, jinsia au eneo au kujihusisha katika kampeni za kusambaza chuki kwenye misingi kama hiyo iliyotajwa;

(b)hakitajihusisha katika au kuchochea ghasia kwa kuwatisha wanachama wake, wafuasi, wapinzani au mtu mwingine yeyote;

(c)hakitaanzisha au kudumisha vikosi vya jeshi la wanamgambo, makundi haramu au mashirika mengine kama hayo;

(d)hakitajihusisha katika utoaji hongo au aina zingine za ufisadi; au

(e)isipokuwa ilivyoelezwa katika Sura hii au katika Sheria ya Bunge, hakitakubali au kutumia rasilimali za umma ili kuimarisha maslahi ya chama au wagombeaji wake katika uchaguzi.

Kif.92

Sheria kuhusu vyama vya kisiasa

Bunge litatunga sheria ili kutoa mwongozo kuhusu—

(a)jukumu la vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali pamoja na aina zingine za vyombo vya utangazaji vilivyotajwa, kugawa sawa muda hewani ambao vyama vya kisiasa vinapewa kijumla au katika kampeni za uchaguzi; na

(b)udhibiti wa uhuru wa kutangaza ili kuhakikisha kampeni zenye haki na usawa wakati wa uchaguzi;

(c)udhibiti wa vyama vya kisiasa;

(d)majukumu ya vyama vya kisiasa;

(e)usajili na usimamizi wa vyama vya kisiasa;

(f)kuundwa na kusimamiwa kwa hazina ya vyama vya kisiasa;

(g)akaunti na ukaguzi wa vyama vya kisiasa;

(h)udhibiti katika matumizi ya rasilimali ya umma ili kuendeleza malengo ya vyama vya kisiasa; na

(i)masuala mengine muhimu katika usimamizi wa vyama vya kisiasa.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho