Katiba ya Kenya, 2010
Sura ya Tisa
Kitengo cha Serikali cha Utendaji
Rais, Naibu wa Rais na Baraza la Mawaziri, na jinsi wanavyochaguliwa au kuteuliwa.
Mamlaka Kuu ya Kitaifa Inayosimamia Utendaji
Sehemu 2Rais na Naibu wa Rais
Uchaguzi wa Rais
(1)Rais—
(a)ndiye Kiongozi wa Taifa na Serikali;
(b)ndiye anayetekeleza mamlaka ya utendaji ya Jamhuri, kwa usaidizi wa Naibu wa Rais na Mawaziri;
(c)ndiye Amiri-Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya;
(d)ndiye mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Usalama; na
(e)ni ishara ya umoja wa kitaifa.
(2)Rais—
(a)ataiheshimu, kuitekeleza na kuilinda Katiba;
(b)ataulinda uhuru wa Jamhuri ya Kenya;
(c)atakuza na kuimarisha umoja wa taifa;
(d)atakuza heshima ya utofauti wa watu najamii za Kenya; na
(3)atahakikisha ulinzi wa haki za kibinadamu na uhuru wa kimsingi, na utawala wa sheria.Rais hatahudumu katika ofisi yoyote nyingine ya Serikali au ya umma.
Majukumu ya Rais
(1)Rais—
(a)atatoa hotuba katika kufunguliwa kwa kila Bunge jipya lililochaguliwa;
(b)atahutubia kikao maalum cha Bunge mara moja kila mwaka na anaweza kuhutubia Bunge wakati mwingine wowote; na
(c)mara moja kila mwaka—
(i)anapohutubia taifa, atatoa ripoti kuhusu hatua zote ambazo zimechukuliwa na maendeleo ambayo yamepatikana katika ufikiaji wa maadili ya kitaifa yanayorejelewa katika Kifungu cha 10;
(ii)atachapisha kwenye Gazeti Rasmi la Serikali maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa na maendeleo chini ya aya ndogo ya (i); na
(iii)atawasilisha ripoti kwa Bunge la Kitaifa ili lijadiliwe kuhusu maendeleo ambayo yamepatikana katika utimizaji wa Jamhuri wa majukumu ya kimataifa. Katiba ya Kenya, 2010 77
(2)Rais atateua, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, atateua kirasmi, na pia anaweza kuwaachisha kazi—
(a)Mawaziri, kwa mujibu wa Kifungu cha 152;
(b)Mwanasheria Mkuu, kwa mujibu wa Kifungu cha 156;
(c)Katibu wa Baraza la Mawaziri, kwa mujibu wa Kifungu cha 154;
(d)Makatibu Wakuu kwa mujibu wa Kifungu cha 155;
(e)makamishna wakuu, mabalozi na wawakilishi wa kidiplomasia; na
(f)kwa mujibu wa Katiba hii, afisa yeyote mwingine wa Serikali au wa umma ambaye kupitia kwa Katiba hii, Rais ana mamlaka ya kumteua au kumwachisha kazi.
(3)Rais—
(a)ataongoza mikutano ya Baraza la Mawaziri;
(b)ataelekeza na kuratibu majukumu ya wizara na idara za serikali; na
(c)kwa uamuzi uliochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali, atagawa majukumu ya utekelezaji wa Sheria ya Bunge kwa Waziri, kwa kiwango ambacho hakikinzani na Sheria yoyote ya Bunge.
(4)Rais anaweza—
(a)kutekeleza jukumu lolote lingine la utendaji lililotolewa katika Katiba hii au katika sheria ya kitaifa na, isipokuwa Katiba hii inapoagiza vinginevyo, anaweza kubuni ofisi katika huduma ya umma kulingana na mapendekezo ya Tume ya Huduma kwa Umma;
(b)kuwapokea mabalozi na wawakilishi wa kidiplomasia wa kigeni;
(c)kutoa tuzo kwa jina la wananchi na la Jamhuri;
(d)kulingana na Kifungu cha 58, kutangaza hali ya dharura; na
(e)kwa idhini ya Bunge, anaweza kutangaza vita.
(5)Rais atahakikisha kwamba majukumu ya kimataifa ya Jamhuri yanatimizwa kupitia kwa utendaji wa Mawaziri husika.
Mamlaka ya Kuwasamehe Waliohukumiwa
(1)Kwa ombi la mtu yeyote, Rais anaweza kutekeleza mamlaka yake ya msamaha kwa mujibu wa ushauri wa Kamati ya Ushauri iliyoundwa chini ya ibara ya (2), kwa—
(a)kumsamehe kabisa au kwa masharti mtu ambaye amepatikana na hatia;
(b)kuahirisha utekelezaji wa adhabu iliyotolewa kwa muda uliowekwa au kwa muda usiojulikana;
(c)kubadili adhabu kwa kiwango kisichokuwa na ukali sana; au
(d)kuondoa adhabu yote au sehemu ya adhabu hiyo.
(2)kutakuwepo Kamati ya Ushauri kuhusu Mamlaka ya Msamaha wa Rais, itakayojumuisha—
(a)Mwanasheria Mkuu;
(b)Waziri anayehusika na huduma za urekebishaji; na
(c)angalau watu wengine watano kama ilivyoagizwa na Sheria ya Bunge, lakini wasiwe maafisa wa Serikali au katika huduma ya umma.
(3)Bunge litatunga sheria ili kutoa mwongozo kuhusu—
(a)muda wa kuhudumu kwa wanachama wa Kamati ya Ushauri;
(b)taratibu za Kamati ya Ushauri; na
(c)vigezo ambavyo vitatumiwa na Kamati ya Ushauri katika kufanya ushauri wake.
(4)Kamati ya Ushauri inaweza kuzingatia maoni ya waathiriwa wa hatia iliyotendwa wanapompendekezea Rais kuhusu msamaha wa hatia hiyo.
Matumizi ya mamlaka ya rais wakati wa urais wa muda mfupi
(1)Mtu ambaye anahudumu kama Rais au yule ambaye ameidhinishwa kwa mujibu wa Katiba hii kutekeleza mamlaka ya Rais—
(a)katika kipindi kinachoanzia mnamo tarehe ya kura ya kwanza kwenye uchaguzi wa rais, na kukamilika wakati Rais mpya aliyechaguliwa anapochukua hatamu za uongozi; au
(b)kwa wakati ambao Rais hayupo au hawezi kutekeleza majukumu yake, au nyakati zingine zilizobainishwa katika kifungu cha 147 (3), hawezi kutekeleza mamlaka ya Rais yaliyotajwa katika ibara ya (2).
(2)Mamlaka yanayorejelewa katika ibara ya (1) ni—
(a)uteuzi au uteuzi rasmi wa majaji wa mahakama ya ngazi juu;
(b)uteuzi au uteuzi rasmi wa afisa yeyote mwingine wa umma ambaye Katiba hii au sheria hii inahitaji ateuliwe rasmi na Rais;
(c)uteuzi au uteuzi rasmi au kuwachishwa kazi kwa Mawaziri na maafisa wengine wa umma au wa Serikali;
(d)uteuzi au uteuzi rasmi au kuachishwa kazi kwa mabalozi au wawakilishi wa kibalozi na kidiplomasia;
(e)mamlaka ya msamaha wa rais; na
(f)mamlaka ya kutoa tuzo kwa jina la wananchi na la Jamhuri.
Maamuzi ya Rais
Uamuzi wa Rais katika utekelezaji wa jukumu lolote la Rais chini ya Katiba hii utakuwa kwa maandishi na utakuwa na muhuri na saini ya Rais.
Uchaguzi wa Rais
(1)Rais atachaguliwa na wapiga kura waliosajiliwa katika uchaguzi wa kitaifa utakaoendeshwa kwa mujibu wa Katiba hii na Sheria yoyote ya Bunge inayosimamia uchaguzi wa rais.
(2)Uchaguzi wa Rais utafanyika––
(a)katika siku sawa na ile ya uchaguzi mkuu wa Wabunge, ikiwa ni siku ya Jumanne ya pili ya mwezi Agosti, katika kila mwaka wa tano; au
Ustahiki na kutostahiki katika kuchaguliwa kama Rais
(1)Mtu anastahiki kuteuliwa kama mgombeaji wa urais ikiwa mtu huyo-—
(a)ni raia kwa kuzaliwa;
(b)anastahiki kugombea uchaguzi kama mwanachama wa Bunge;
(c)ameteuliwa na chama cha kisiasa au ni mgombea huru; na
(d)ameteuliwa na wapiga kura wasiopungua elfu mbili kutoka kila kaunti kwa idadi kubwa ya kaunti hizo.
(2)Mtu hastahiki kuteuliwa kama mgombea wa urais ikiwa mtu huyo-—
(a)ameuweka uaminifu wake katika taifa la kigeni; au
(b)ni afisa wa umma, au anahudumu katika ofisi yoyote ya Serikali au ya umma.
(3)Ibara ya (2) (b) haitatumika kwa—
(a)Rais;
(b)Naibu wa Rais; au
(c)Mbunge.
Mchakato wa uchaguzi wa rais
(1)Ikiwa ni mgombea mmoja wa urais atakayeteuliwa, mgombeaji huyo atatangazwa kuwa amechaguliwa.
(2)Ikiwa ni wagombeaji wawili wa urais watakaoteuliwa, uchaguzi utafanyika katika kila eneobunge.
(3)Katika uchaguzi wa rais—
(a)watu wote waliosajiliwa kama wapiga kura kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge wana haki ya kupiga kura;
(b)uchaguzi utakuwa kwa njia ya siri katika siku ambayo imeelezewa chini ya ibara ya 101 (1) na kwa wakati, mahali na kwa njia ambayo imeagizwa chini ya Sheria ya Bunge; na
(c)baada ya kuhesabiwa kwa kura katika vituo vya kupigia kura, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itahesabu na kuhakikisha hesabu ya kura na kutangaza matokeo.
(4)Mgombea wa urais atatangazwa kuchaguliwa kama Rais ikiwa mgombea huyo atapokea—
(a)zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo; na
(b)angalau asilimia ishirini na tano ya kura zilizopigwa katika kila kaunti, katika zaidi ya idadi nusu ya kaunti zote.
(5)Ikiwa hakuna mgombea atakayechaguliwa, uchaguzi mwingine utafanyika upya katika kipindi cha siku thelathini baada ya uchaguzi uliopita, na katika uchaguzi huo mpya, wagombeaji watakuwa tu—
(a)mgombea au wagombea ambao walipokea kura nyingi zaidi; na
(b)mgombeaji au wagombeaji ambao walipata idadi kubwa ya pili ya idadi ya kura.
(6)ikiwa wagombea zaidi ya mmoja atapokea idadi kubwa zaidi ya kura, ibara ya (5) (b) haitatumika na wagombeaji watakaokuwa katika uchaguzi mpya watakuwa wale ambao wamebainishwa katika ibara ya (5) (a).
(7)mgombeaji atakayepokea idadi kubwa zaidi ya kura katika uchaguzi mpya ndiye atakayetangazwa kuwa Rais.
(8)uchaguzi wa urais utafutiliwa mbali na uchaguzi mwingine mpya kufanyika ikiwa—
(a)hakuna mtu ambaye ameteuliwa kama mgombea kabla ya kumalizika kwa kipindi kilichowekwa cha kuwasilisha walioteuliwa;
(b)mgombeaji wa uchaguzi wa Rais au wa Naibu wa Rais atafariki katika au kabla ya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi; au
(c)mgombea uchaguzi ambaye alistahili kutangazwa kuwa amechaguliwa kama Rais, atafariki kabla ya kutangazwa kuwa amechaguliwa kama Rais.
(9)Uchaguzi mpya wa urais chini ya ibara ya (8) utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya tarehe iliyokuwa imewekwa ya uchaguzi uliopita.
(10)Katika muda wa siku saba baada uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka—
(a)atangaza matokeo ya uchaguzi; na
(b)atawasilisha taarifa iliyoandikwa ya matokeo ya uchaguzi kwa Jaji Mkuu na Rais aliye mamlakani.
Kifo kabla ya kuchukua hatamu
(1)Ikiwa aliyetangazwa kuwa Rais-mteule atafariki dunia kabla ya kuchukua hatamu za uongozi––
(a)Naibu wa Rais-mteule ataapishwa kama Rais wa muda mfupi mnamo tarehe ile ambayo Raismteule angeapishwa; na
(b)uchaguzi mpya wa Rais utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya kifo cha Rais-mteule.
(2)Ikiwa Naibu wa Rais-mteule atafariki kabla ya kuchukua hatamu za uongozi, kiti cha Naibu wa Rais kitatangazwa kuwa wazi baada ya Rais-mteule kuchukua hatamu za uongozi.
(3)Ikiwa watu wote wawili waliotangazwa kuchaguliwa kama Rais pamoja na Naibu wa Rais watafariki kabla ya kuchukua hatamu za uongozi––
(a)Spika wa Bunge la Kitaifa atakuwa Rais wa muda mfupi kuanzia siku ambayo Rais mteule angeapishwa; na
(b)uchaguzi mpya utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya kifo cha pili.
Maswali kuhusu uhalali wa uchaguzi wa rais
(1)Mtu anaweza kuwasilisha ombi au malalamishi katika Mahakama ya Juu Zaidi ili kupinga uchaguzi wa Raismteule katika muda wa siku saba baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.
(2)Katika muda wa siku kumi na nne baada ya kuwasilishwa kwa ombi au malalamishi, Mahakama ya Juu Zaidi itasikiza na kuamua kesi hiyo na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.
(3)Ikiwa Mahakama ya Juu Zaidi itaamua kuwa uchaguzi wa Rais mteule sio halali, uchaguzi mpya utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya uamuzi huo.
Kuchukua hatamu za Urais
(1)Kuapishwa kwa Rais Mteule kutafanyika wazi na mbele ya Jaji Mkuu, au, ikiwa Jaji Mkuu hayupo, mbele ya Naibu Jaji Mkuu.
(2)Rais mteule ataapishwa Jumanne ya kwanza itakayofuata––
(a)siku ya kumi na nne baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais, ikiwa hakuna kesi ya malalamishi iliyowasilishwa mahakamani chini ya Kifungu cha 140; au
(b)siku ya saba kufuatia tarehe ambayo mahakama itatoa uamuzi na kutangaza kuwa uchaguzi ulikuwa halali, ikiwa kesi ya malalamishi iliwasilishwa chini ya Kifungu cha 140.
(3)Rais-mteule anachukua hatamu za uongozi kwa kula kiapo au kutoa uthibitisho wa uaminifu; na kiapo au uthibitisho wa kutekeleza majukumu ya ofisi kama ilivyoabainishwa katika Ambatisho la Tatu.
(4)Bunge, kupitia kwa sheria, litatoa taratibu za sherehe za kuapishwa kwa Rais-mteule.
Muda wa kuhudumu katika ofisi ya Rais
Ulinzi dhidi ya mashtaka
(1)Mashtaka yoyote ya jinai hayatafunguliwa au kusikizwa katika mahakama yoyote dhidi ya Rais au yeyote ambaye atakuwa anatekeleza majukumu ya ofisi hiyo wakati wa uongozi wake.
(2)Mashtaka katika kesi za madai hayatawasilishwa katika mahakama yoyote dhidi ya Rais au yeyote anayetekeleza majukumu ya ofisi hiyo kwa wakati wa uongozi wake, kutokana na chochote kilichofanywa au kutofanywa katika utekelezaji wa mamlaka yake chini ya Katiba hii.
(3)Iwapo mwongozo umetolewa katika sheria ili kudhibiti muda ambao mashtaka yanaweza kuwasilishwa dhidi ya mtu chini ya ibara ya (1) au (2), kipindi cha muda ambao mtu huyo anahudumu au kutekeleza majukumu ya ofisi ya Rais hazitazingatiwa katika kuhesabu kipindi cha wakati ambao umeagizwa na sheria hiyo.
(4)Kinga dhidi ya kushtakiwa kwa Rais katika Kifungu hiki, haitatumika kwa hatia ambayo Rais anaweza kushtakiwa chini ya mkataba wowote ambao Kenya imetia saini na ambao unatupilia mbali kinga hiyo.
Kuondolewa kwa Rais kwa misingi ya kukosa uwezo
(1)Mwanachama wa Bunge la Kitaifa anaweza kuwasilisha hoja Bungeni, ya kuchunguzwa kwa uwezo wa afya ya kiakili au ya kimwili ya Rais katika kutekeleza majukumu ya ofisi yake ikiwa ataungwa mkono na robo ya idadi ya wabunge wote.
(2)Ikiwa hoja chini ya ibara ya (1) itaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa—
(a)Spika wa Bunge atamjulisha Jaji Mkuu kuhusu uamuzi huo katika kipindi cha siku mbili; na
(b)Rais ataendelea kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo kabla ya matokeo ya taratibu zinazohitajika katika Kifungu hiki.
(3)Katika muda wa siku saba baada ya kupokea notisi ya uamuzi huo kutoka kwa Spika, Jaji Mkuu atateua kikundi cha watu watakaosikiza na kuamua swala hilo, ikijumuisha—
(a)watu watatu ambao wanastahiki kuhudumu kama matabibu chini ya sheria za Kenya, na walioteuliwa na taasisi ambayo kwa kisheria inawajibika katika kudhibiti taaluma ya utabibu;
(b)wakili mmoja wa Mahakama Kuu aliyeteuliwa na taasisi ambayo kisheria inawajibika katika kudhibiti utendakazi katika taaluma ya mawakili; na
(c)mtu mmoja atakayeteuliwa na Rais.
(4)Ikiwa Jaji Mkuu atashindwa kuteua kikundi hiki chini ya ibara ya (3) , Naibu Jaji Mkuu atakiteua kikundi hicho.
(5)Ikiwa Rais atashindwa kumteua mtu anayehitajika kuteuliwa chini ya ibara ya (3) (c), mtu huyo atateuliwa na––
(a)mwanafamilia katika familia ya Rais; au
(b)ikiwa hakuna mwanafamilia yeyote ambaye yuko tayari au ana uwezo wa kufanya uteuzi huo, uteuzi huo utafanya na jamaa wa karibu wa Rais.
(6)Kikundi hicho kitachunguza suala hilo na kuripoti kwa Jaji Mkuu na Spika wa Bunge la Kitaifa katika muda wa siku kumi na nne baada ya kuteuliwa.
(7)Spika atawasilisha ripoti hiyo ya kikundi kilichoteuliwa mbele ya Bunge la Kitaifa katika kipindi cha muda wa siku saba baada ya kuipokea.
(8)Ripoti hiyo ya kikundi kilichoteuliwa itakuwa ya mwisho na isiyoweza kukatiwa rufaa na ikiwa kikundi hicho kitaripoti kwamba Rais ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo, Spika wa Bunge la Kitaifa atatangaza ripoti hiyo katika Bunge la Kitaifa.
(9)Ikiwa kikundi hicho kitaripoti kwamba Rais hana uwezo wa kutekeleleza majukumu ya ofisi hiyo, Bunge la Kitaifa litapiga kura ya kuidhinisha au kutoidhinisha ripoti hiyo.
(10)Ikiwa idadi kubwa ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa watapiga kura ya kuunga mkono kuidhinishwa kwa ripoti hiyo, Rais atang’atuka mamlakani.
Kuondolewa kwa Rais kupitia kura ya kutokuwa na imani
(1)Mwanachama katika Bunge la Kitaifa, iwapo ataungwa mkono na thuluthi moja ya wabunge wote, anaweza kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rais—
(a)kwenye msingi wa ukiukaji mkubwa wa Kifungu cha Katiba hii au sheria nyingine yoyote;
(b)ikiwa kuna sababu muhimu za kuamini kwamba Rais amehusika katika uhalifu chini ya sheria za kitaifa au kimataifa; au
(c)kwenye msingi wa mwenendo mbaya zaidi ofisini.
(2)Ikiwa thuluthi mbili ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa wataunga mkono hoja chini ya ibara ya (1)—
(a)Spika atamuarifu Spika wa Bunge la Seneti kuhusu uamuzi huo katika muda wa siku mbili; na
(b)Rais ataendelea kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo kabla ya matokeo ya taratibu zinazohitajika katika Kifungu hiki.
(3)Katika kipindi cha siku saba baada ya kupokea notisi ya uamuzi kutoka kwa Spika wa Bunge la Kitaifa—
(a)Spika wa Seneti ataandaa mkutano wa Seneti ili kusikia mashtaka dhidi ya Rais; na
(b)Bunge la Seneti, kwa uamuzi wake, linaweza kuteua kamati maalum itakayojumuisha maseneta kumi na moja ili kuchunguza suala hilo.
(4)Kamati maalum iliyoteuliwa chini ya ibara ya (3) (b)—
(a)itachunguza suala hilo; na
(b)kuripoti kwa Seneti katika muda wa siku kumi ikiwa tuhuma dhidi ya Rais zimethibitishwa kwa maoni ya Kamati hiyo.
(5)Rais atakuwa na haki ya kufika na kuwakilishwa mbele ya Kamati hiyo maalum wakati wa uchunguzi.
(6)Ikiwa Kamati Maalum itaripoti kwamba maelezo yaliyotolewa katika tuhuma dhidi ya Rais—
(a)hayajathibitishwa, hakuna usikilizaji zaidi utakaoendelea chini ya Kifungu hiki unaohusiana na tuhuma hizo.
(b)yamethibitishwa, Bunge la Seneti litapiga kura katika mashtaka ya kutokuwa na imani baada ya kumpa Rais nafasi ya kusikizwa.
(7)Ikiwa angalau thuluthi mbili ya wanachama wote wa Seneti watapiga kura ya kukubaliana na mashtaka ya kutokuwa na imani, Rais ataondoka ofisini.
Nafasi Katika Ofisi ya Rais
(1)Ofisi ya Rais itakuwa wazi ikiwa anayehudumu katika ofisi hiyo—
(a)Atafariki dunia;
(b)atajiuzulu kwa kumwandikia barua Spika wa Bunge la Kitaifa; au
(c)atakapoondoka ofisini vinginevyo chini ya Kifungu cha 144 au cha 145 au chini ya Kifungu kingine cha Katiba hii.
(2)Nafasi inapotokea katika ofisi ya Rais—
(a)Naibu wa Rais atahudumu kama Rais kwa muda uliosalia wa muhula wa Rais; au
(b)Ikiwa kuna nafasi katika ofisi ya Naibu wa Rais, au Naibu wa Rais hawezi kuhudumu kama Rais, Spika wa Bunge la Kitaifa atahudumu kama Rais na uchaguzi wa urais utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya nafasi hiyo kutokea katika ofisi ya Rais.
(3)Mtu atakayehudumu kama Rais chini ya ibara ya (2) (a) au kufuatia uchaguzi unaohitajika chini ya ibara ya (2) (b), isipokuwa aondolewe mamlakani kwa mujibu wa Katiba hii, ataendelea kuhudumu kama Rais hadi wakati ambapo Rais aliyechaguliwa upya aapishwe baada ya uchaguzi unaofuatia kama ilivyoratibiwa chini ya Kifungu cha 136 (1).
(4)Ikiwa Naibu wa Rais atahudumu kama Rais chini ya ibara ya (2) (a) au mtu achaguliwe kuwa Rais chini ya Ibara ya (2) (b), Naibu wa Rais au mtu huyo aliyechaguliwa atachukuliwa kwa madhumuni ya Kifungu cha 142 (2) kuwa—
(a)amehudumu kama Rais kwa muhula mzima ikiwa katika tarehe
(b)ambayo mtu huyo alianza kuhudumu, kumesalia zaidi ya miaka miwili na nusu kabla ya tarehe ya uchaguzi ulioratibiwa kikawaida chini ya Kifungu cha 136 (2) (a); au
(c)hajahudumu kama Rais kwa muhula mzima katika hali ingine yoyote.
Majukumu ya Naibu wa Rais
(1)Naibu wa Rais ndiye atakayekuwa msaidizi mkuu wa Rais na atakuwa kaimu wa Rais katika utekelezaji wa majukumu ya Rais.
(2)Naibu wa Rais atatekeleza majukumu yaliyotolewa na Katiba hii na majukumu mengine yoyote ya Rais ambayo Rais anaweza kutoa.
(3)Kwa mujibu wa Kifungu cha 134, wakati ambapo Rais hayupo au hawezi kutekeleza majukumu yake kwa muda mfupi, na katika kipindi kingine chochote ambacho Rais anaweza kuamua, Naibu wa Rais atahudumu kama Rais.
(4)Naibu Rais hatahudumu katika ofisi nyingine ya Serikali au ya umma.
Kuchaguliwa na Kuapishwa kwa Naibu wa Rais
(1)Kila mgombea katika uchaguzi wa urais atateua mtu ambaye anastahiki kuteuliwa kuwa mgombeaji wa urais, kama mgombeaji wa kiti cha Naibu wa Rais.
(2)Kwa madhumuni ya ibara ya (1), hakutakuwa na mchakato tofauti wa kumteua Naibu wa Rais na Kifungu cha 137 (1) (d) hakitatumika kwa mgombea wa kiti cha Naibu wa Rais.
(3)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itamtangaza mgombeaji aliyeteuliwa na mtu ambaye amechaguliwa kuwa Rais, kuwa amechaguliwa kama Naibu wa Rais.
(4)Kuapishwa kwa Naibu wa Rais mteule kutafanyika mbele ya Jaji Mkuu, au iwapo Jaji Mkuu hayupo, mbele ya Naibu wa Jaji Mkuu na kwa uwazi.
(5)Naibu wa Rais mteule atachukua hatamu za uongozi kwa—
(a)kula kiapo au kutoa uthibitisho wa uaminifu; na
(b)Kula kiapo au kutoa uthibitisho wa kutekeleza majukumu ya ofisi,kama ilivyoagizwa katika Ambatisho la Tatu.
(6)Muhula wa kuhudumu kama Naibu wa Rais utaanzia tarehe ya kuapishwa kwa Naibu wa Rais, na utakamilika—
(a)wakati ambapo mtu atakayechaguliwa kuwa Rais anayefuata katika uchaguzi chini ya Kifungu cha (136) (2) (a) ataapishwa;
(b)Naibu wa Rais anapohudumu kama Rais; au
(c)kwa kijiuzulu, kufariki au kuondolewa mamlakani kwa Naibu wa Rais.
(7)Naibu wa Rais anaweza, kwa wakati wowote, kujiuzulu kwa kumwandikia barua Rais na kujiuzulu huko kutatekelezeka katika saa na tarehe iliyobainiwa katika barua hiyo, au ikiwa tarehe haijabainishwa, adhuhuri ya siku ifuatayo baada ya kupokelewa kwa barua hiyo.
(8)Hakuna mtu yoyote atakayehudumu kama Naibu wa Rais kwa zaidi ya mihula miwili.
Nafasi Katika ofisi ya Naibu wa Rais
(1)Katika muda wa siku kumi na nne baada ya nafasi kutokea katika ofisi ya Naibu wa Rais, Rais atamteua mtu mwingine kuijaza nafasi hiyo, na Bunge la Kitaifa litapiga kura kuhusu uteuzi huo katika muda wa siku sitini baada ya kuupokea.
(2)Ikiwa mtu atahudumu kama Naibu wa Rais chini ya ibara ya (1), basi, kwa madhumuni ya Kifungu cha 148 (8), mtu huyo atachukuliwa—
(a)kuwa amehudumu katika muhula mzima kama Naibu wa Rais ikiwa, kwa wakati ambao mtu huyo alianza kuhudumu katika ofisi hiyo, zaidi ya miaka miwili na nusu inasalia kabla ya uchaguzi unaofuatia ulioratibiwa chini ya Kifungu cha 136 (2); au
(b)hajahudumu kama Rais kwa muhula mzima katika hali ingine yoyote.
Kuondolewa kwa Naibu wa Rais
(1)Naibu wa Rais anaweza kuondolewa ofisini—
(a)kwenye msingi wa kutokuwa na uwezo wa kiakili au kimwili wa kutekeleza majukumu ya ofisi; au
(b)kwa kura ya kutokuwa na imani—
(i)kwenye msingi wa kukiuka Katiba hii au sheria yoyote nyingine;
(ii)iwapo kuna sababu kuu za kuamini kwamba Naibu wa Rais amefanya uhalifu chini ya sheria ya kitaifa au ya kimataifa; au
(iii)kwenye msingi wa mwenendo mbaya zaidi ofisini.
(2)Sheria katika Vifungu vya 144 na 145 vinavyohusiana na kuondolewa mamlakani kwa Rais, kwa kuzingatia mabadiliko yanayostahili, itatumika katika kumuondoa Naibu wa Rais.
Malipo na manufaa ya Rais na Naibu wa Rais
(1)Mshahara na manufaa ambayo Rais na Naibu wa Rais watapata utatolewa kwenye Hazina Jumuishi.
(2)Malipo, manufaa na haki maalum wanazopata Rais na Naibu wa Rais hayatabadilishwa kwa lengo la kutowanufaisha wakiwa ofisini.
(3)Malipo ya uzeeni anayopaswa kulipwa Rais mstaafu na Naibu wa Rais mstaafu pamoja na haki maalum na marupurupu mengine wanayopata hayatabadilishwa ili kutowanufaisha katika maisha yao yote.
Sehemu 3Baraza la Mawaziri
Baraza la Mawaziri
(1)Baraza la Mawaziri linajumuisha—
(a)Rais;
(b)Naibu wa Rais;
(c)Mwanasheria Mkuu; na
(d)Mawaziri wasiopungua kumi na wanne au wasiozidi ishirini na wawili.
(2)Rais atawapendekeza, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa kuwateua Mawaziri.
(3)Waziri hatakuwa Mbunge.
(4)Kila mtu atakayeteuliwa kama Waziri—
(a)ataanza kuhudumu kwa kuapa au kutoa thibitisho la uaminifu kwa watu na Jamhuri ya Kenya na kuapa kuitii Katiba hii, mbele ya Rais na kwa mujibu wa Ambatisho la Nne; na
(b)anaweza kujiuzulu kwa kumwasilishia Rais taarifa iliyoandikwa ya kujiuzulu kwake.
(5)Rais––
(a)anaweza kubadilisha wizara ambayo Waziri atahudumu;
(b)anaweza kumwachisha kazi Waziri; na
(c)atamwachisha kazi Waziri iwapo atahitajika kufanya hivyo, kwa uamuzi uliokubaliwa chini ya ibara ya (6) hadi (10).
(6)Mwanachama wa Bunge la Kitaifa anayeungwa mkono na angalau robo moja ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa, anaweza kupendekeza hoja wa kumtaka Rais amwachishe kazi Waziri—
(a)kwenye msingi wa ukiukaji mkubwa wa Kifungu cha Katiba hii au sheria nyingine yoyote;
(b)Iwapo kuna sababu kuu za kuamini kwamba Waziri huyo amefanya uhalifu chini ya sheria ya kitaifa au ya kimataifa; au
(c)kwa msingi wa mwenendo mbaya zaidi ofisini.
(7)Ikiwa hoja chini ya ibara ya (5) itaungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa—
(a)Bunge la Kitaifa litateua kamati maalum akayojumuisha wanachama kumi na mmoja kuchunguza suala hili; na
(b)katika muda wa siku kumi, kamati hii maalum itaripoti kwa Bunge la Kitaifa ikiwa limepata madai dhidi ya Waziri kuthibitishwa.
(8)Waziri ana haki ya kufika au kuwakilishwa mbele ya kamati maalum wakati wa uchunguzi wake.
(9)Ikiwa kamati hiyo maalum itaripoti kwamba imepata madai hayo
(a)othibitishwa, hakuna taratibu zingine zitakazofuatwa; au
(b)kuthibitishwa, Bunge la Kitaifa––
(i)litampa Waziri nafasi ya kusikizwa; na
(ii)litapiga kura ili kuidhinisha uamuzi unaomtaka Waziri kuachishwa kazi.
(10)Ikiwa uamuzi ulio chini ya ibara ya (8) unaomtaka Rais kumwachisha kazi Waziri utaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa––
(a)Spika atamwasilishia Rais uamuzi huu kwa haraka; na
(b)Rais atamwachisha kazi Waziri huyo.
Maamuzi, majukumu na kuwajibika kwa Baraza la Mawaziri
(1)Uamuzi wa Baraza la Mawaziri utakuwa kwa maandishi.
(2)Mawaziri wanawajibika kibinafsi na kwa pamoja kwa Rais katika utekelezaji wa mamlaka yao na utendakazi wa majukumu yao.
(3)Waziri atahudhuria kikao cha kamati ya Bunge la Kitaifa au Seneti, anapohitajiwa na kamati, na kujibu swali lolote kuhusu suala linalomhusu.
(4)Mawaziri––
(a)watatekeleza majukumu yao kulingana na Katiba hii; na
(b)watawasilisha kwa Bunge ripoti kamili na za mara kwa mara kuhusu masuala yaliyo chini ya udhibiti wao.
Katibu wa Baraza la Mawaziri
(1)Ofisi ya Katibu katika Baraza la Mawaziri imebuniwa, ambayo ni ofisi katika huduma ya umma.
(2)Katibu katika Baraza la Mawaziri—
(a)atapendekezwa, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa kuteuliwa na Rais; na
(b)anaweza kuachishwa kazi na Rais.
(3)Katibu katika Baraza la Mawaziri—
(a)atasimamia ofisi ya Baraza la Mawaziri;
(b)atakuwa na jukumu la kupanga shughuli na kuweka kumbukumbu za mikutano ya Baraza la Mawaziri, kulingana na maelekezo ya Baraza hilo;
(c)atawasilisha uamuzi wa Baraza la Mawaziri kwa watu au mamlaka zinazofaa; na
(d)atakuwa na majukumu mengine kama atakavyoelekezwa na Baraza la Mawaziri.
(4)Katibu katika Baraza la Mawaziri anaweza kujiuzulu kwa kutoa notisi kwa njia ya maandishi, kwa Rais.
Makatibu Wakuu
(1)Ofisi ya Katibu Mkuu limebuniwa, ambayo ni ofisi katika huduma ya umma.
(2)Kila idara ya Serikali itakuwa chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu.
(3)Rais—
(a)atapendekeza mtu ili ateuliwa kama Katibu Mkuu kutoka miongoni mwa wale watakaopendekezwa na Tume ya Huduma za Umma; na
(b)atawateua Makatibu Wakuu kwa idhini ya Bunge la Kitaifa.
(4)Rais anaweza kubadilisha idara ambayo itasimamiwa na Katibu Mkuu.
(5)Katibu Mkuu anaweza kujiuzulu kwa kumwandikia Rais notisi.
Sehemu 4Ofisi Zinginezo
Mwanasheria Mkuu
(1)Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Imebuniwa.
(2)Mwanasheria Mkuu atapendekezwa na Rais, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, kuteuliwa na Rais.
(3)Ustahiki katika kuteuliwa kama Mwanasheria Mkuu ni sawa na wa kuteuliwa katika ofisi ya Jaji Mkuu.
(4)Mwanasheria Mkuu—
(a)ndiye mshauri mkuu wa kisheria katika Serikali.
(b)atawakilisha Serikali ya kitaifa mahakamani au katika kesi zinginezo za kisheria ambazo serikali ya kitaifa inahusika, isipokuwa kesi za jinai; na
(c)atatekeleza majukumu mengine yoyote yatakayotolewa na Sheria ya Bunge au Rais.
(5)Mwanasheria Mkuu atakuwa na mamlaka, kwa ruhusa ya mahakama, ya kuisaidia mahakama katika kutatua kesi za uraia ambazo Serikali sio mhusika.
(6)Mwanasheria Mkuu ataukuza, kuulinda na kuutetea utawala wa sheria na kutetea maslahi ya umma.
(7)Mamlaka ya Mwanasheria Mkuu yanaweza kutekelezwa kibinafsi au kupitia kwa maafisa wasaidizi watakaotekeleza majukumu hayo kulingana na maagizo maalum au ya kijumla.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma
(1)Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imebuniwa.
(2)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atapendekezwa na Rais, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, atateuliwa na Rais.
(3)Ustahiki wa kuteuliwa kama Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ni sawa na zile wa uteuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu.
(4)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atakuwa na mamlaka ya kumwagiza Inspekta Jenerali wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa kuchunguza habari yoyote au madai ya vitendo vya jinai, na Inspekta Jenerali huyo atafuata maelekezo hayo.
(5)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atahudumu kwa muhula wa miaka minane na hatastahiki kuteuliwa tena.
(6)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atatekeleza mamlaka ya Serikali ya kufungua mashtaka na anaweza—
(a)kufungua mashtaka katika kesi ya uhalifu dhidi ya mtu yeyote katika mahakama yoyote (isipokuwa mahakama ya kijeshi) kutokana na kosa lolote linalodaiwa kufanywa;
(b)kuchukua na kuendeleza kesi zozote ya uhalifu zilizoanzishwa katika mahakama yoyote (isipokuwa katika mahakama ya kijeshi) na ambazo zilifunguliwa au kusimamiwa na mtu mwingine au mamlaka nyingine; na
(c)kwa mujibu wa ibara ya (7) na (8), kusitisha, kwa wakati wowote kabla ya hukumu kutolewa, kuendelea kwa kesi zozote za jinai, zilizowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma au kuendelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya umma chini ya aya ya (b)
(7)Ikiwa kusitishwa kwa kesi zozote chini ya ibara ya (6) (c) kutafanyika baada ya upande wa mashtaka kufunga kesi yao, mshtakiwa ataachiliwa huru.
(8)Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma hawezi kusitisha kuendelea kwa kesi bila ruhusa ya mahakama.
(9)Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma yanaweza kutekelezwa naye kibinafsi au kupitia kwa maafisa wasaidizi watakaotekeleza mamlaka hayo kulingana na masharti maalum au ya kijumla.
(10)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma hatahitaji idhini ya mtu au mamlaka yoyote ili kuwasilisha kesi za kijinai, na katika kutekeleza mamlaka au majukumu yake hataelekezwa au kudhibitiwa na mtu au mamlaka yoyote.
(11)Katika kutekeleza mamlaka yaliyotolewa na Kifungu hiki, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atazingatia maslahi ya umma, utekelezaji wa haki na hitaji la kuzuia na kuepuka matumizi mabaya ya mchakato wa kisheria.
(12)Bunge linaweza kutunga sheria itakayotoa mamlaka ya kufungua mashtaka kwa taasisi zingine kando na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.
Kuondolewa na kujiuzulu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma
(1)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kuondolewa ofisini kwenye misingi ya—
(a)kutoweza kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo kutokana na kukosa uwezo wa kiakili au wa kimwili;
(b)kutozingatia Sura ya Sita;
(c)kufilisika;
(d)kutokuwa na uzoefu unaohitajika; au
(e)mwenendo mbaya zaidi ofisini au tabia mbaya.
(2)Mtu anayetaka kuondolewa mamlakani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kuwasilisha ombi au malalamishi kwa Tume ya Huduma za Umma ambayo yatakuwa kwa njia ya maandishi, yakiainisha madai yanayounda msingi wa kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.
(3)Tume ya Huduma za Umma itajadili malalamishi hayo na ikiridhika kwamba yanafichua kuwepo kwa msingi wa kuondolewa ofisini chini ya Ibara ya (1), itawasilisha ombi au malalamishi hayo kwa Rais.
(4)Baada ya kupokea na kuchunguza ombi au malalamishi hayo, Rais, katika muda wa siku kumi na nne, atamsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kabla ya hatua kuchukuliwa na Rais kulingana na ibara ya (5) na kwa ushauri wa Tume ya Huduma za Umma, atateua kikundi cha watu watakaosikiza na kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo, itakayojumuisha—
(a)wanachama wanne kutoka miongoni mwa wale ambao wanahudumu au wamewahi kuhudumu kama majaji katika mahakama ya ngazi ya juu, au wanaostahiki kuteuliwa kuwa majaji katika mahakama ya ngazi ya juu;
(b)wakili mmoja ambaye amehudumu kwa angalau miaka kumi na mitano na atakayeteuliwa na taasisi ya kisheria inayowajibika katika udhibiti wa taaluma ya mawakili; na
(c)watu wengine wawili walio na uzoefu katika masuala ya umma.
(5)Kikundi hicho kitachunguza swala hilo kwa haraka na kuripoti kuhusu ukweli uliopo na kutoa mapendekezo kwa Rais, ambaye atachukua hatua kulingana na mapendekezo ya kikundi hicho.
(6)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ambaye amesimamishwa kazini kulingana na ibara ya (4) atapokea nusu ya mshahara wake hadi atakapoondolewa au kurudishwa ofisini kwake.
(7)Kikundi kitakachoteuliwa chini ya ibara ya (4) kitamchagua mwenyekiti miongoni mwao wanachama wake.
(8)Kikundi kitakachoteuliwa chini ya ibara ya (4) kitakuwa na jukumu la kudhibiti taratibu zake.
(9)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kujiuzulu kwa kumwandikia Rais notisi.