(1)Kila mtu ana haki ya kutaka mzozo wowote unaoweza kusuluhishwa kisheria kuamuliwa katika kikao kilicho wazi na chenye usawa mahakamani au, ikiwezekana, kuamuliwa na taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama, iliyo huru na isiyoegemea upande wowote.
(2)Kila mshtakiwa ana haki ya kesi yake kusikizwa kwa njia ya haki, ambayo inajumuisha haki ya—
(a)kuchukuliwa kama asiyekuwa na hatia hadi itakapothibitishwa kuwa ana hatia;
(b)kuarifiwa kuhusu mashtaka na kupewa maelezo ya kutosha na yatakayomwezesha kujibu mashtaka hayo;
(c)kuwa na wakati na vifaa vya kutosha ili kutayarisha jibu;
(d)kesi kusikilizwa kwa njia ya uwazi mbele ya mahakama iliyobuniwa chini ya Katiba hii;
(e)kesi kuanzishwa na kukamilishwa pasi na kuchelewa bila sababu;
(f)kuwepo wakati wa kesi kusikizwa isipokuwa pale ambapo mienendo ya mshtakiwa inatatiza kuendelea kwa kesi hiyo;
(g)kuchagua na kuwakilishwa na wakili, na kuelezwa kuhusu haki hii haraka iwezekanavyo;
(h)kuwa na wakili aliyetolewa na Serikali na kwa gharama ya Serikali, ikiwa haki haitatendeka, na aarifiwe kuhusu haki hii haraka iwezekanavyo;
(i)kunyamaza kimya na kutotoa ushahidi katika usikilizaji wa kesi;
(j)kuelezwa mbeleni kuhusu ushahidi ambao kiongozi wa mashtaka ananuia kutumia, na kuweza kuufikia ushahidi huo;
(k)kuleta na kupinga ushahidi;
(l)kukataa kutoa ushahidi utakaopelekea yeye kupatikana na hatia;
(m)kuwa na usaidizi wa mkalimani bila malipo ikiwa mshtakiwa hawezi kuelewa lugha inayotumiwa katika kesi yake;
(n)kutohukumiwa kwa kitendo ambacho kwa wakati wa kutendeka kwake kitendo hicho hakikuwa—
(i)kosa nchini Kenya; au
(ii)kosa la jinai chini ya sheria ya kimataifa;
(o)kutoshtakiwa kwa kosa ambalo mtu huyo amewahi kutenda, kuachiliwa au kuhukumiwa kwalo hapo awali;
(p)kunufaika katika kupata adhabu iliyo na ukali wa chini zaidi kati ya adhabu zilizoruhusiwa katika kosa hilo ikiwa adhabu iliyoidhinishwa kwa kosa lake imebadilishwa kati ya muda wa kutendeka kwa kosa hilo na wakati wa kuhukumiwa; na
(q)ikiwa atahukumiwa, kukata rufaa au kuwasilisha ombi la kukaguliwa kwa uamuzi huo katika mahakama iliyo katika kiwango cha juu kuliko mahakama iliyotoa uamuzi kama inavyobainishwa na sheria.
(3)Ikiwa Kifungu hiki kinahitaji maelezo au habari kutolewa kwa mtu, maelezo hayo yatatolewa katika lugha ambayo mtu huyo anaelewa.
(4)Ushahidi uliopatikana katika njia inayokiuka haki yoyote au uhuru wowote wa kimsingi katika Sheria za Haki utatengwa ikiwa mahakama kuukubali ushahidi huo kutapelekea kesi hiyo kutozingatia haki, au kwa namna nyingine ushahidi huo utazuia kutendeka kwa haki.
(5)Mshtakiwa—
(a)aliyeshtakiwa kwa kosa fulani, kando na kosa ambalo mahakama inaweza kukamilisha kwa haraka, atakuwa na haki ya kupata nakala ya kumbukumbu ya kesi aombapo nakala hiyo; na
(b)ana haki ya kupata nakala ya kumbukumbu ya kesi ndani ya muda unaofaa baada ya kukamilishwa kwa kesi hiyo, na kwa malipo ya ada inayofaa kama ilivyoagizwa na sheria.
(6)Mtu aliyehukumiwa kwa kosa la jinai anaweza kuwasilisha ombi la kusikizwa upya kwa kesi katika mahakama kuu ikiwa––
(a)rufaa ya mtu huyo imetupiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi ambapo mtu huyo ana haki ya kukata rufaa, au ikiwa mtu huyo hakukata rufaa katika muda unaokubaliwa wa kukata rufaa; na
(b)ushahidi mpya na wa kushawishi umepatikana.
(7)Ili haki itendeke, mahakama inaweza kumruhusu mtu tofauti kumsaidia mlalamishi au mshtakiwa ili awasiliane na mahakama.
(8)Kifungu hiki hakizuii kutengwa kwa vyombo vya habari au umma katika kesi yoyote mahakamani, ikiwa kutengwa huko ni muhimu, katika jamii huru na ya kidemokrasia, ili kulinda mashahidi au watu walio hatarini, kulinda maadili, utulivu wa umma, au usalama wa kitaifa.
(9)Bunge litatunga sheria itakayoelezea kuhusu ulinzi, haki na maslahi ya waathiriwa wa hatia.