Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Moja · Serikali ya Ugatuzi

Kifungu cha 192

Kif.192

Kusimamishwa kwa serikali ya kaunti

(1)Rais anaweza kusimamisha serikali ya kaunti kwa muda—

(a)katika hali ya dharura inayotokana na mzozo wa kindani au vita; au;

(b)katika hali zingine maalum.

(2)Serikali ya kaunti haitasimamishwa kwa muda chini ya ibara ya (1) (b) isipokuwa tume huru imefanya uchunguzi wa madai dhidi ya serikali ya kaunti, Rais ameridhika kwamba madai hayo yamethibitishwa na Seneti imeidhinisha kusimamishwa huko.

(3)Kwa wakati ambao serikali ya kaunti imesimamishwa kwa muda chini ya Kifungu hiki, mikakati itawekwa ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya serikali ya kaunti kulingana na Sheria ya Bunge.

(4)Kwa wakati wowote, Seneti inaweza kutupilia mbali kusimamishwa huko.

(5)Kusimamishwa kwa muda chini ya Kifungu hiki hakutaendelea kwa zaidi ya kipindi cha siku tisini.

(6)Kipindi kilichotolewa chini ya ibara ya (5) kinapokamilika, uchaguzi wa serikali ya kaunti husika utafanyika.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Moja →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho