Utekelezwaji wa haki za mazingira
(1)Ikiwa mtu atadai kuwa haki ya kupata mazingira safi na yenye afya njema inavyotambuliwa na kulindwa chini ya Kifungu cha 42 imekiukwa, inakiukwa au kuna uwezekano mkubwa wa mtu huyo kunyimwa haki hiyo au haki hiyo kukiukwa, kuvunjwa au kutishiwa, mtu huyo anaweza kuwasilisha kesi mahakamani ili kupata fidia pamoja na hatua zingine za kisheria zinazopatikana katika suala hilo.
(2)Ikiwa ombi litawasilishwa chini ya sehemu ya (1), mahakama inaweza kutoa amri, au kutoa maelekezo yoyote ambayo yanafaa––
(a)ili kuzuia, kukomesha au kusitisha tendo au kosa lolote ambalo ni hatari kwa mazingira;
(b)ili kumshurutisha afisa yeyote wa umma kuchukua hatua zitakazozuia au kusitisha tendo au kosa lolote ambalo ni hatari kwa mazingira; au
(c)kutoa fidia kwa mwathiriwa yeyote aliyeathirika kutokana na ukiukaji wa haki ya kupata mazingira safi na yenye afya njema.
(3)Kwa madhumuni ya Kifungu hiki, sio lazima kwa anayewasilisha ombi kuonyesha kwamba mtu yeyote amepata hasara au kujeruhiwa.